Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Rizki Pemba Juma akiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Simai Mohammed Said, wakisalimiana na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja |
Sekta ya Utalii ni moja ya sekta ambazo serikali ya Zanzibar imekuwa ikizitegemea
katika ukusanyaji wa kodi, ni sekta ya Biashara, sekta ya Utalii, Viwanda,
nyumba za kulala wageni na starehe yaani pamoja na sekta nyengine mbali
mbali ambazo zinatambulika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Licha ya sekta hizo na nyengine nyingi kuwa ni sehemu ya tegemeo la
serikali katika ukusanyaji wa fedha ambazo hutumikwa kwa ajili ya kuleta
maendeleo ya jamii, lakini kwa upande mwengine baadhi ya sekta hizo uwepo wake
bila ya kuangaliwa vyema uendeshaji wake ni wazi kuwa zinaweza kuleta athari
makubwa kwa jamii hasa watoto ambao ndio tegemeo la kesho.
Moja ya sekta hizo ni sekta ya Biashara ya nyumba za kulala wageni na
starehe yaani Baa, hasa kwa zile Baa zinazoanzishwa pembezoni au karibu na
makaazi ya wananchi au karibu ya shule hasa za watoto wadogo yaani shule za
msingi za kati pamoja na Secondary.
Ni dhahiri kuwa pasi na usimamizi ulio bora wa uanzishwaji wa Baa
athari kwa watoto kuacha masomo au kutofikia malengo yanahitajika katika
upatikanaji wa elimu bora kwa watoto walio chini na umri wa miaka 18 wakiwamo
wanaume na wanawake.
Pamoja na athari za baa kuwepo katika maeneo mengi lakini katika
Makala haya nimeanagazia Mkoa wa Kusini Unguja, katika Wilaya ya Kusini ambapo
kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012 Wilaya ya Kusini Unguja
ina jumla ya wakaazi 39,242 wakiwamo wanaume 19,342 na wanawake 19,900 .
Licha ya biashara hiyo kuwa kuna baadhi ya watu wanaikubali lakini
wananchi walio wengi katika Wilaya hiyo pamoja na viongozi mbali mbali pamoja
na wadau na wanaharakati wamekuwa wakizilalamikia kutokana na maadili ya watoto
kuanza kupotea kidogokidogo.
Wazazi wazungumzia suala
hilo
Baadhi wananchi wamesa ni jambo la kusikitisha sana kuona kila uchao
katika Wilaya hiyo ongezeko la Baa maeneo yasiostahiki ikiwamo maeneo ya karibu
na shule limekuwa linazidi, hali ambayo imeanza kuleta athari kwa watoto wao
wadogo hasa wale walioanza kuoma shule.
Mmoja wananchi hao ambao hakupendwa kutajwa jina lake gazetini
kutokana na sababu zake za msingi alisema baadhi ya watoto wao tayari wameanza
kuathirika kitabia kutokana na uwepo wa Baa hizo, ziliomo maeneo ya karibu na
makaazi pamoja na Shule.
Alisema baadhi ya watoto tayari wamebadilika wengine wameanza
kujiingiza katika matumizi ya vinywaji vya ulevu na wengine wamo katika kundi
vitendo vya ngono.
Alisema jitihada mbali mbali wameweza kuchukua ili kuona Baa hizo
zinasimamishwa kazi lakini hadi sasa hakuna mafanikio yaliopatikana, licha ya
kundi la watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuanza kubadilika kimaadili.
“Mtoto anakuanga anaenda shule kumbe hafiki shule anamalizia Baa,
inasikitisha sana kwani wakati wowote watoto wanaweza kuathirika hata kiafya,
tunaamini hali hii inaweza kuondoka pindi serikali ikachukua hatua madhubuti
juu ya wamiliki wa Baa”alisema.
Kwa upande baadhi ya wanafunzi nao hawakunya nyuma kulisemea hilo,
ambapo walidai kuwa ni ukweli kwamba uwepo wa baa maeneo ya karibu na Shule
kunawaathiri sana kielimu kutokana na kelele zikiwamo za walevi pamoja mavazi
ya wasichana wanaotumia baa hizo.
Wadau wazungumza
Mmoja wadau wakubwa wanaoguswa na kadhia hiyo ni Kaimu Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Kizimkazi Mkunguni, Mah-fudh Said Omar alisema licha ya jitihada kubwa
wanayochukua juu ya ufundishaji wananafunzi lakini kuwepo kwa Baa hizo
kunachangia kwa kiasi kubwa kutofikia malengo yao,akidai kuwa baadhi ya
wanafunzi huacha kabisa kuendelea na masomo kutokana na kuathiriwa na Baa hizo.
Alisema
kuwepo kwa baa hizo baadhi ya wanafunzi hushawishika kujiingiza katika vitendo
viovu, ikiwamo unywaji ulevi pamoja na vitendo vya uasharati, hali
inayochangiwa na wigo kutoka kwa watumiaji wa Baa hizo kijijini hapo.
“Kiukweli
halii hii huchangia kushuka kwa kiwango cha elimu kwa wanafunzi wetu, hivyo ni
vyema kwa taasisi husika kulitafutia ufumbuzi tatizo hili ili kuona vijana wetu
wananufaika vema na elimu, pamoja na kuifanya shule yetu kupata matokeo mazuri
ya mitihani”alisema.
Naye Mjumbe wa kamati kuu ya Wapinga Baa Zanzibar, Seif Omar Seif
amefahamisha kuwa baa nyingi zilizopo nchini zipo karibu na makaazi ya watu
jambo linalopelekea kuhatarisha usalama wa watoto.
Alisema
wao kama wapinga Baa mara nyingi huchukua jitihada za kutoa elimu kwa jamii
hasa katika kipindi cha utoaji wa leseni za Baa, kwenda Mahakani ili kupinga
uwepo wa Baa hizo ila kinachotokea ni baadhi ya wananchi kushindwa kujitokeza
kwa wingi katika kuweka pingamizi.
Alisema
pindi wananchi wakiungana kwa pamoja hasa kwa kuweka pingamizi ya kupatiwa
leseni, ni suluhisho kubwa la kusitisha Baa hizo, akidai kuwa kinyume chake
wanaweza kutumia muda mwingi wa kulalamika bila ya kupata muafaka kwa wakati.
Kwa
upande wa Afisa Sheria kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela)
Khadija Mabrouq Hassan alisema kitendo cha ujenzi wa Baa karibu ya maeneo ya
shule hakikubaliki hata kidogo, hivyo aliwaomba wananchi kuungana kwa pamoja
kuweka pingamizi ya utolewaji wa vibali muda utakapowadia.
Alisema
anaamini wazi kuwa pingamizi za wananchi zinaweza kushinda kutokana na
mapangamizi yao yanweza kuwa na mashiko makubwa hasa kutokana na Baa hizo kuwa
karibu ya Shule za wanafunzi.
Baadhi ya wamiliki wa Baa hizo walidai kuwa wamekua wakifanya jitihada
mbali mbali za kuhakikisha Baa hizo hazina athari kwa watoto, wakidai kuwa
kutokana na jitihada hizo ndio maana huopatiwa vibali vya kuendelea na biashara
hiyo.
Viongozi wa Serikali
wasema
Naye
kaimu Sheha wa Shehia hiyo, Suleiman Ameir Juma alisema uongozi wa Shehia hiyo
upo tayari kushirikiana na wazazi na wananchi wa eneo hilo katika kuhakikisha
suala la elimu kwa watoto linathaminiwa kwa maslahi ya jamii na taifa kwa
ujumla.
Alisema
katika kulitilia mkazo suala hilo uongozi wa Shehia kwa kushirikiana na
wananchi umepanga utaratibu wa kuwaendeleza na masomo ya elimu mbadala
wanafunzi 250 walioacha masomo katika kijiji hicho chenye wakaazi 4,250.
Kwa upande wa Afisa Wanawake Wilaya ya Kusini, Haji Choum Haji alisema
kutokana na uwepo wa hali hiyo wamekuwa wakifanya jitihada mbali mbali, ikiwamo
kutoa elimu kwa watoto, kukaa na wadau mbali mbali, kuzungumza na wazazi pamoja
na kutumia njia mbali mbali ili kuona watoto wanaishi katika mazingira bora.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud akizungumzia kadhia
hiyo alisema ni kweli serikali imekuwa ikitoa vibali vya uendeshaji wa Baa, ila
wananchi nao wana haki ya kupinga Baa hizo kila muda unapofika wa kuomba vibali
kwa wafanyabishara hao.
Alisema kwa upande wa Serikali ya Mkoa huo baada ya kubaini tatizo
hilo wameamua kuunda kamati ndogo ya usalama ili kukagua pamoja na kutoa
mapendekezo yao kwa kamati ya Mkoa ya usalama ili kama kuna hatua za kuchukua
ifanyike hivyo kwa mujibu wa sheria.
Alisema hawafurahii hata kidogo kuona hivi sasa Mkoa wa Kusini kuwa ni
moja ya Mkoa unaoasemeka vibaya juu ya athari za watoto ikiwamo kujiingiza
katika vitendo vya ngono.
Kwa upande wa Mkurugenzi Elimu ya Maandalizi, Msingi na Kati Safia
Rijali alisema tayari Wizara yake imepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa
Wilaya hiyo juu ya uwepo wa kadhia hiyo na kuahidi kuwa hatua madhubuti
zitachukuli za ufatiliaji.
Makala imeandaliwa na Haji M. Mohd, chini ya ufadhili wa UNICEF
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment