Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kimemsimamisha kazi Muamuzi Mfaume Ali Nassor kwa muda mpaka pale Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) watakapotoa taarifa za uchunguzi unaendelea dhidi ya Waamuzi wanne wa Tanzania ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa.

Mfaume Ali Nassor ni miongozi mwa Waamuzi wa Tanzania waliochezesha mchezo namba 54 wa ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya LLB ACADEMIC ya Burundi dhidi ya RAYON SPORTS ya Rwanda ambao kwasasa wako hatarini kufungiwa na shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kama watakutwa na hatia ya upangaji wa matokeo katika mchezo uliomalizika kwa RAYON SPORTS kushinda kwa 1-0 ugenini na kufuzu katika hatua nyengine.

Hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania TFF kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake Wilfred Kidao limethibitisha kupokea barua kutoka CAF kufanyiwa uchunguzi waamuzi hao.

Kidao alisema kama waamuzi hao wakipatikana na hatia, waadhibiwe ipasavyo na kama wakiwa hawana hatia waachiwe huru.

Waamuzi hao ni Mfaume Ali Nasoro ambae ni Muamuzi wa kati, Frank John Komba muamuzi msaidizi namba 1, Sudi Lila muamuzi msaidizi nambari 2 na Israel Mujuni muamuzi wa akiba ndiyo watuhumiwa kwenye tuhuma hizo na imeelezwa kuwa viongozi wa Rayon Sports walionekana kwenye moja ya chumba cha mwamuzi usiku wa kuamkia siku ya mchezo wenyewe, kitu ambacho kilizua tafrani kwenye hotel waliyokuwa wamefikia waamuzi hao na baadhi ya wageni (RAYON SPORTS) kukamatwa na polisi.

Msimamizi wa mchezo huo uliofanyika Februari 21 mwaka huu naye alikuwa katika hotel hiyo hiyo na kutokana na purukushani hizo alitoka nje na kuangalia hali ilivyokuwa inaenda ambapo aliandika ripoti yenye maelezo ya kilichotokea pamoja na ushahidi wa video za CCTV tayari kwa uchunguzi.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top