Shamra shamra za sherehe za maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia uzinduzi na uwekaji wa Mawe ya Msingi ya Miradi tofauti ya Kiuchumi na Maendeleo zilizoanza Rasmi  Jumapili ya Tarehe 31 Disemba Mwaka Jana  hivi sasa zinakaribia kufikia ukingoni.

Maandalizi ya kilele cha sherehe hizo zinazojumuisha Vikosi vya Ulinzi na Usalama Nchini sambamba na Maandamano ya Wananchi wa Mikoa Mitano ya Zanzibar yamekamilika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika pamoja na Makamanda wa Vikosi vya Ulinzi Nchini wameshuhudia Maandalizi hayo ya mwisho ya Gwaride linalotarajiwa kupamba sherehe za Kilele cha Maadhimisho hayo zilizofanyika katika Uwanja wa Aman Mjini Zanzibar.



Gwaride hilo limewaunganisha Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ}, Polisi, Kikosi cha Kuzuia Magendo {KMKM}, Mafunzo. Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU}, Kikosi cha Valantia {KVZ} pamoja na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar {KZUZ}.

Askari hao  Mwaka huu wamepunguza  baadhi ya vitendo vinavyopamba Gwaride hilo ikiwemo Mwendo wa Pole kwa kuzingatia kwamba Tarehe 12 Januari imesimama Siku Tukufu ya Ujumaa ambapo Waumini wa Dini ya Kiislamu wamezingatiwa kupatiwa muda wa  kwenda kushiriki Sala ya Ijumaa.

Viongozi na Makamanda hao  wameonyesha kuridhika kwao  na ukakamavu ulioonyeshwa  na Askari wa Vikosi vinavyoshiriki Gwaride hilo la Maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  ya Mwaka 1964 yaliyoondoa madhila ya kutawaliwa.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Halmashauri  ya Sherehe  na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema ameridhika na maandalizi hayo na kuwashauri wasimamizi wa sherehe hizo kuzingatia vyema muda uliowekwa.

Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo alisema Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar imeamua Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 55 kuzifanyia Kisiwani Pemba.

Aliwataka wahusika wote kuhakikisha kwamba wanazingatia maandalizi ya awali ili kuhakikisha sherehe hizo zinafanikiwa na kupambika kama matarajio  yaliyokusudiwa na Serikali Kuu.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi wa Pemba kulipokea mapema wazo hilo la Serikali kwa kufanya maandalizi mapema  kwa lengo la kupunguza gharama  zinazoweza kuepukwa.

Wakichangia mbinu na mikakati ya kufanikisha sherehe hizo baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo walisema ushiriki wa Wananchi katika Sherehe hizo umezingatiwa na kupewa umuhimu wa pekee ambapo Serikali inafahamu wazi kwamba wao ndio wadau wa mwanzo katika Sherehe hizo.

Walisema katika kuzingatia muda muda wa Kilele cha maadhimisho hao Viongozi wanaosimamia matukio tofauti uwanjani wanapaswa kwenda na Ratiba bila ya kuingiza kitu chochote  kwa nia ya kuheshimu mpangilio wote.

Kilele cha Sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kinatarajiwa kuhitimishwa Januari 12 katika Uwnja wa Aman Siku itakayokuwa mapumziko ili kuwapa fursa Wananchi kushiriki vyema kwenye sherehe hizo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kulihutubia Taifa Uwanjani hapo Hotuba itakayorushwa Moja kwa  moja kupitia Vyombo mbali mbali vya Habari Nchini ikiwemo pia Mitandao ya Kijamii itakayowapa nafasi Walimwengu Duniani kushuhudia Sherehe hizo.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top