Bi Safia Nassor Mbarouq akiwa na mtoto wake Arafat Makame Yussuf pamoja na wajuu zake

“Ndoto zangu za kuwa na familia yenye wasomi zilizimika rasm mnamo miaka ya 2000, baada ya mume wangu kunipa talaka pamoja na kuniwachia ulezi wa watoto wanane peke yangu hali ya kuwa sikuwa na kazi ya kuajiriwa wala kujiari”.

Hiyo ni kauli ya huzuni ya Bi Safia Nassor Mbarouq (59) mkaazi wa Masingini Wilaya ya Magharib ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, ambaye bado ana ndoto za kuwa na familia yenye masomi bora pindi akipata msaada wa kusomeshewa watoto wake .

Alisema kabla ya ndoa yake kuvunjika alikuwa na matumaini mazuri ya watoto wake kupata elimu bora, kutokana na mashirikiano mazuri aliyonayo kati yake na mumewe wakati wawapo ndani ya ndoa hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10.

Alisema licha ya mumewe kutokuwa na uwezo mkubwa kifedha ila walikuwa wanaishi katika mazingira mazuri ya kuelewana, ila ghafla mumuwe huyo alianza kubadilika tabia kidogo kidogo hatimae kufikia maamuzi ya kumpa talaka.

“Licha ya talaka kuwa na maumivu yake lakini maumivu makubwa niliyoyapata baada ya kunipa talaka aliniamuru kuodoka na watoto wangu, hali ambayo ilinifanya kutoamini kilichotokea ila niliamini, hasa kwa kuwa tayari ameshaniacha”alisema.

Aliongeza kusema kuwa “Nilitamani watoto niwaache lakini kutokana na machungu ya uzazi nililazimika kuwachukuwa watoto wangu wote licha ya kuwa ninapokwenda sijui nitafikia wapi mimi pamoja na watoto wangu wote”alisema.

Kuanza maisha mapya

Bi Safia ambaye ni mzanzibar lakini alikuwa ameolewa jijiji Dar es Sallam anasema baada ya kupewa talaka ilimlazimu kufungisha kila kilicho chake na kurudi zake Zanzibar ambako ndio nyumbani kwao.

“Sikuweza kurudi katika nyumba za ndugu zangu wa familia kutokana wao wenyewe maisha yao ni duni, nilianza kuhangaika kutafuta sehemu ya kukaa ila nashukuru nilipa nyumba eneo la Mwera ambayo nilikodoshwa kwa njia ya msaada maana fedha nilizokuwa natoa haziendani na malipo halisi ya kodi”alisema.

Alisema maisha ya hapo hayakuwa ya kudumu kwani baada ya kipindi mwenye nyumba alitaka nyumba yake na alitafuta sehemu yenyengine ya kujihifadhi yeye na watoto wake maeneo ya huko huko Mwera Wila ya Magharib ‘B’ Unguja.

“Hadi sasa nimeshakaa katika nyumba sita zote ni sawa na kuazimwa tu maana baadhi huambiwa nilipe japo hela ndogo na nyengine huekwa bure kama mlinzi tu wa nyumba hizo ambazo nyingi huwa zimo katika harakati za ujenzi”alisema.

Bi Safia ambaye hivi sasa anaishi maeneo ya Mwera Masingini katika nyumba ya kuazimwa yeye pamoja na watoto wake anasema bado akili yake haijatulia vyema hasa kwa kuwa hadi wakati huu hana sehemu ya uhakika ya kuishi yeye pamoja na familia yake.

Harakati za kutafuta maisha

Bi Safia anasema licha ya kupata hifadhi katika nyumba mbali mbali lakini suala la chakula pamoja na elimu kwa watoto wake lilikuwa ni gumu sana hasa kwa kuwa yeye ndio alikuwa ni mama na baba wa watoto hao hasa kwa kuwa baba wa watoto hao hakuwa na msaada hata kidogo.

Alisema licha ya kufanya mawasiliano nae lakini hakukuwa na msaada hata kidogo kwa watoto wake hao, ni yeye mwenyewe alikuwa anapambana kwa kufanya kila aina ya kazi ili kuona watoto wake wanapata mlo japo mmoja kwa siku.

“Sikuwa na kazi maalum hadi hii leo, kazi yangu wakati mwengine ni kutafuta vibarua vya kuuza mama ntilie au kubanja kokoto (kubanja mawe) na kuuza kwa watu wanaojenga,nashukuru huwa napata alau pesa”alisema.

Anasema  kutokana na ukali wa maisha, alifanya mawasiliano na dada wa aliyekuwa mumewe ambaye alikuwa naishi Dar es Sallam, lengo ni kutaka msaada, hatiamae ombi lake lilikubaliwa.

Anasema Wifi yake huyo alikuwabali kuwachukuwa watoto wawili kati ya nane alionao kwa lengo la kuwalea ili kumpunguzia ulezi, kitendo ambacho kilimpa faraja kiasi.

“Nashukuru wifi yangu huyo aliwachukua tangu wadogo hadi sasa wamefikia kidatu cha tatu, ila hivi karibuni ameshafariki dunia, hivyo watoto wangu hivi sasa wapo huko huko Dar es Sallam kwa jamaa zao ila hawaendelei na masomo, kutokana na aliyekuwa akiwalipia ameshafariki na hakuna aliyejitokeza kuwaendeleza na masomo hadi sasa”alisema kwa huzuni.

Anasema kwa upande wa watoto anaoendelea kuwalele yeye ni mtoto mmoja tu ambaye amefikia elimu ya kidato cha nne ambaye alifanya mitihani yake mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2019, na hivi sasa anasubiri matokeo.

Alisema watoto wake wengine wanatano hakuweza kupata elimu vyema,kutokana na changamoto za kimaisha ila bado ana matumaini wanaweza kusoma pindi akijitokeza mtu au taasisi itakayomuunga mkono katika malezi.

“Kwa sasa sitamaini ndoa hata kidogo na naichukukia kabisa, ninachotamani ni kuona watoto wangu wanakuwa na elimu ili wawe msaada kwangu”alisema.

Bi Safia mwenye watoto nane wakiwamo sita wanawake na wawili wanaume ambapo mtoto wa mwanzo anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 na wa mwisho ana miaka 16, anasema hawezi kukaa mbali na watoto wake hao hata kidogo ijapokuwa hali ya maisha ni ngumu.

Anasema licha ya kutamani kupita katika vyombo vya sheria pamoja na taasisi mbali mbali za kuisheria ili kumsaidia tatizo lakino hilo lakini amekuwa akikosa kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa mtu wa kumuongoza kufanya hivyo.

“Natamanai sana kufika katika maeneo ya kisheria ili kudai haki ya malezi kutokana na aliyekuwa mume wangu lakini sina mtu wa kuniongoza, kwani mimi mwenyewe muda mwingi nimekuwa napambana na utafutaji wa maisha’alisema.

Mmoja watoto wa Bi Safia, Arafat Makame Yussuf alisema kiukweli maisha wanayoishi ni magumu hivyo aliomba jamii kutoa misaada kwa upande wao hasa katika suala la elimu pamoja na makaazi ambayop ni muhimu katika kuwa na maisha ya uhakika.

Naye Afisa Sheria kutoka chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar (Zafela), Khadija Mbarouk Hassan alisema kwa mujibu wa sharia ya mtoto namba 6 ya mwaka 2011, utelekezaji au udhalilishaji wa mtoto ni kosa kisheria na mtendaji anastahiki kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema wao kama cha cha wanasheria wanawake ambao mara nyingi hutetea wanawake na watoto wamekuwa wakifanya jitihada mbali mbali za utatuzi wa migogoro ya kindoa ikiwamo malezi kwa wato wote.

Alisema kinachotakiwa kwa wananchi hasa wanawake wanaopata matatizo ya kindoa kufika katika ofisi zao ili kueleza kilichowakuta, hatimae uongozi wa Zafela utachukua jitihada za usaidia wake kama inavyofanya, lengo ni kuona haki inatendeka.

Alisema katika kuhakikisha wanatoa msaada kwa jamii wameanzisha wasaidizi wa Sheria Wilaya ambao kazi yao ni kukusanya taarifa za matukio hayo, hivyo ni vyema wananchi hasa wanawake kuwatumia wasaidizi hao ili kupata msaada kwa mujibu wa shida za kisheria walizonazo.

Kwa upande wa aliyekuwa Mume wa Bi Safia, Makame Yussuf akizungumzia mkasa huo alisema sababu kuu ya kuachana na mkewe huyo ni yeye baada ya kuongeza mke wa pili ndipo Bi Safia aliamua kudai kuachwa na ndipo yalipofikia maamuzi ya kuachana.

Alisema baada ya kuachana naye Bi Safia alichukua maamuzi ya kuondoka na watoto, kutokana na hasira ila Makame alidai kuwa hakusita kutoa msaada pamoja na ushirikiana nae kwa hali na mali pale unapohitajika licha ya kuwa walikuwa wameshaachana.

Alisema kwa kuwa tayari wameshaachana hawezi kutoa msaada mkubwa kama walivyokua pamoja ndani ya ndoa, ila pale unapohitajika msaada wake hasa kwa watoto wake huwa tayari kutoa.

Makame alisema kuwa kwwa kuwa wameshaachana hawezi kufatilia maisha yake ya wapi anaishi au wanaishi vipi, ila kikubwa anashukuru alikaa nae vyema ndani ya ndoa na hawezi kusitisha mahusiano yake mema ya kusaidiana hasa kwa kuwa tayari wameshazaa .

Imeandikwa na Haji M. Mohd, chini ya ufadhili wa UNICEF

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top