HOTUBA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI; MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA KWANZA WA KAMATI
YA MAWAZIRI WENYE DHAMANA YA MENEJIMENTI YA MAAFA
KWA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA MAENDELEO
KUSINI MWA AFRIKA, MADINAT AL BAHR - ZANZIBAR
21 FEBRUARI, 2020

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mhesimiwa Zubeir Ali Maulid,  Spika wa  Baraza la  Wawakilishi Zanzibar
Mheshimiwa, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu;
Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, 
Waheshimiwa Mawaziri Mliohudhuria hapa,
Mheshimiwa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Katibu Mtendaji, Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika;
Mheshimiwa, Dkt Thembinkosi Mhlongo, Naibu Katibu Mtendaji, Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika;
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Mabodi;
Ndugu Makatibu Wakuu;
Ndugu Manaibu Makatibu Wakuu;
Washiriki wote wa Mkutano huu;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana,

Assalam Aleikum,

Namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa kila kitu,  kwa kutujaaliya afya njema na kutuwezesha  kuwepo hapa kwa ajili ya kufanya Mkutano huu wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa. Natoa shukurani zangu za dhati kwa  Kamati ya Maandizi ya Mkutano huu kwa mafanikio makubwa. Naithamini sana heshima hii kubwa mliyonipa ya kuwa Mgeni Rasmi wa Mkutano huu.  Ahsanteni sana.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimejiandaa vizuri kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mkutano huu muhimu unafanyika kwa ufanisi mkubwa. Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar, natoa shukurani za dhati kwa Uongozi wa Kamati ya Maandalizi na uongozi wote wa SADC kwa kuichagua Zanzibar kuwa mahali pa kuufanyia mkutano huu.  Kwa hakika uamuzi wenu wa kuja Zanzibar kuufanya mkutano huu, unatoa fursa nzuri kwa wananchi wa Zanzibar ya  kuyafahamu kwa undani zaidi  majukumu na umuhimu wa Jumuiya ya SADC.

Tunakukaribisheni Zanzibar nyote wageni waalikwa kutoka nchi mbali mbali. Itumieni vizuri fursa hii ya kushiriki katika mkutano huu, kwa kufanya ziara za matembezi, ili muone mandhari nzuri ya Zanzibar, vivutio vya utalii, fukwe zilizopo na maeneo mbali mbali ya historia pamoja na Mji Mkongwe, ambao ni urithi wa Kimataifa. Zanzibar ina historia kubwa yenye kuwavutia wageni kutoka mataifa yote duniani, ambayo imekuwa ikijulikana na ikipendwa kwa uzuri wake wa kimaumbile, ucheshi na ukarimu wa watu wake pamoja na ustaarabu wa kuishi kwa kushirikiana na kuvumiliana mambo yaliyodumu tangu kale na dahari.

Zanzibar  hivi sasa ni miongoni mwa nchi na vituo maarufu vya kufanyia mikutano, semina na makongamano ya Taasisi za Kimataifa. Naamini kwamba  Jumuiya ya SADC pamoja na  taasisi mbali mbali za Serikali na zile za binafsi zilizo katika umoja huu zitaendelea kufanya mikutano yao Zanzibar kwa kuzingatia sifa ilizonazo  na huduma zinazotolewa na hoteli zilizopo hapa, kama  hii ya Madinat Al Bahr. Tuzingatie hekima ya usemi maarufu wa Kiswahili usemao  Mramba asali harambi mara moja’.   Kwa hivyo, safari hii mliokuja isiwe mwisho, bali muwe mnakuja mara kwa mara, hata kwa kupumzika na familia zenu.  Zipo hoteli za kila daraja zenye kutoa huduma bora kwa bei nafuu, kwa kampuni na familia mbali mbali.  KARIBUNI SANA.

Ndugu Washiriki,
Nimevutiwa sana na ajenda kuu ya Mkutano huu iliyomo kwenye  kaulimbiu isemayo: "Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.”  Hapana shaka tangu mkutano huu ulipoanza, tarehe 18 hadi leo, masuala mengi muhimu yanayohusu maafa  tayari yameshajadiliwa  kwa kuzingatia Kaulimbiu hii.

Ilivyokuwa maafa ni matukio yanayoleta hasara kubwa kwa taifa lolote kutokana na  majanga yanayoambatana nayo, ajenda na kauli mbiu ya mkutano huu zimesadifu sana katika lengo kuu la mkutano huu. Mijadala iliyofanywa na itakayoendelea hivi leo, yote imelenga katika kulifanikisha lengo hilo,  katika hali ya kuimarisha ushirikiano na  kuchochea ari na  juhudi zilizopo, ili kupambana na  kupunguza athari za maafa. Mkakati wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Kikanda wa mwaka 2016 - 2030,  pamoja na kuridhia Mfumo Mkakati wa  Kuhimili Maafa  wa Kikanda wa mwaka 2020 - 2025, mtakayoijadili katika mkutano huu, ni mambo muhimu.  Umuhimu wake upo katika  utekelezaji wa mipango  ya kuhimili maafa ya kitaifa na ya Kimataifa inayoendelea kutekelezwa na nchi wanachama, ukiwemo Mkakati wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa wa mwaka 2015 - 2030  (The Sendai Framework for Disaster Risk Reduction 2015–2030), uliojadiliwa  mjini Sendai - Japan na baadae  ukapitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka  2015.

Vile vile,  naamini kwamba mazungumzo yaliyofanyika kwa lengo la kujenga mustakbali mwema juu ya masuala mbali mbali yanayohusu matumizi ya Mfuko wa Fedha za Ufadhili wa Mabadiliko ya Tabianchi, yamefikia hatua nzuri na maazimio yatakayopitishwa yatanzingatia maslahi  ya  nchi zote wanachama na maendeleo ya SADC kwa jumla.

Mkutano huu ni muhimu, tukijua kwamba  washiriki nyote mna uwezo na  ushawishi mkubwa katika nchi zenu  wa kuyaingiza  masuala ya kukabiliana na maafa katika mipango ya maendeleo, mipango ya  kisekta, miradi inayofadhiliwa na wahisani mbali mbali pamoja  na mipango mengine ya kiutawala. Mmepewa dhamana ya kuyashughulikia masuala yanayohusu maafa,yanayosimamiwa na Jumuia hii, kutokana na sifa zenu maalum mlizonazo. Sifa ambazo zimeonesha  umahiri, uwezo na uzoefu wenu  mkubwa katika  kupanga na kuitekeleza mikakati ya kujiandaa, kukabiliana na kuirejesha hali ya maisha ya wananchi  baada ya kukumbwa na  maafa; pamoja na kujikinga na kupunguza matukio ya maafa.

Ndugu Washiriki,
Kufanyika kwa Mkutano huu ni hatua muhimu katika kujenga matumaini mapya ya wananchi kuhusiana na maafa, tukizingatia kwamba katika miaka ya hivi karibuni  kumekuwa na ongezeko kubwa la  maafa pamoja na viashiria  vyake  katika nchi wanachama wa SADC. Maafa hayo yanatokana na matukio mbali mbali ya kimaumbile na yasiyokuwa ya kimaumbile yakiwemo yale ya vimbunga na dhoruba, matetemeko ya ardhi, ukame, moto wa misituni, mafuriko, miripuko ya maradhi na ajali za baharini na barabarani.  Matukio mengine husababishwa na wadudu waharibifu wa mazao, uchafuzi wa mazingira, ongezeko la kina cha bahari, uvamizi wa maji ya chumvi na matukio mengine yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na matumizi mabaya ya rasilimali tulizojaaliwa. Maafa yanayotokana na mambo yote hayo husababisha upotevu wa maisha, mali za watu na uharibifu wa miundombinu; na hivyo yanaathiri sana ajenda za maendeleo zinazopangwa kutekelezwa na nchi zetu.

Ndugu Washiriki,
Takwimu za utekelezaji wa “Mkakati wa Sendai” zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2015 na 2018, Ukanda wa SADC umepata zaidi ya matukio 160 ya maafa. Maafa hayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000, na yameathiri watu milioni 22. Kadhalika, maafa hayo yalileta uharibifu mkubwa, ambao gharama  zake zilikadiriwa kuwa  ni  Dola za Kimarekani bilioni 3.7.  Athari mbaya za matukio ya maafa haziko katika gharama za kifedha tu zinazotumika,  bali zina madhara makubwa ya kisaikolojia kwa jamii zilizoathirika. Tunapoangalia upande wa hasara kifedha, tutaona kwamba gharama ya Dola za Kimarekani bilioni 3.7. ni kubwa, tukizingatia kwamba bado nchi zetu zinahitaji fedha kwa  ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu mipya badala ya kuijenga tena ile iliyokuwa imeshajengwa. Nchi zetu zinahitaji fedha katika kuimarisha huduma za afya, elimu, maji safi na salama, kilimo, elimu, ujenzi wa miundombinu na uwekezaji katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Kwa hivyo, kwa kuzingatia athari za maafa zinazogharimu maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi zetu, ni lazima Jumuia ya SADC iwe na mipango na mikakati imara ya  kupambana na maafa, hasa yale yanayotokea mara kwa mara.  Kwa hivyo, ni lazima tujipange vizuri kwa kuandaa  mikakati imara ya kuvitambua na kuviwahi viashiria vipya vya maafa kila vinapoanza kujitokeza. Kwa  mfano, Kamati hii ina nafasi ya kutoa maelekezo na mapendekezo juu ya nini kifanyike kwa  ngazi ya kitaifa na kikanda, ili tuweze  kujikinga na  maradhi mapya yaliyoingia ya Virusi vya Corona (Covid-19), ambayo tayari yameshaenea katika nchi mbali mbali.  Ni lazima tuwe na mipango ya kukabiliana nayo katika kila hali.  Vile vile, changamoto ya nzige iliyojitokeza hivi karibuni katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambao wanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya  kilimo na usalama wa chakula katika baadhi ya  nchi, ni suala ambalo linahitaji kuzungumzwa na kupangiwa mikakati ya pamoja. Wahenga wanasema Tahadhari kabla ya athari.’ Naamini kwamba haya ni miongoni mwa majukumu ya Kamati  hii inayoshughulika  na masuala ya maafa.

Ndugu Washiriki,
Ni dhahiri kwamba, katika muda huu wa siku nne,  washiriki katika ngazi mbali mbali mmepata  muda wa kutosha wa kujadili na kubainisha uzoefu  katika masuala na matukio  mbali  mbali yanayohusu maafa. Vile vile,  tumemsikia  Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, alivyoelezea  matukio  mbali mbali ya  maafa yaliyotokezea katika nchi za SADC na atahari  zake  kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi wanachama.
Kwa hivyo, itakuwa ni vyema na mimi nikaelezea angalau kwa ufupi  juu ya juhudi na mipango ya Serikali yetu ya  Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maafa. Kabla sijatoa maelezo yanayohusu Zanzibar, nataka niseme kwa jumla juu ya uzoefu katika changamoto zinzozikabili nchi za visiwa.

Ndugu Washiriki,
Mara nyingi watu wanaoishi katika visiwa  wamo  hatarini zaidi  ya kukabiliwa na  maafa, hasa katika wakati huu ambapo dunia imekabiliwa na changamoto nyingi zinazotakana na mabadiliko ya tabianchi.  Miongoni mwao ni ongezeko la kina cha maji ya bahari, jambo ambalo linasababisha maeneo mengi  kuvamiwa na maji ya chumvi, na hatimae kuathiri makaazi na shughuli za kilimo.

Baadhi ya wakati, wananchi wanapoteza maisha  yao kwa usafiri wa baharini na shughuli za uvuvi hasa unapotokea upepo mkali na  kimbunga.  Hivi sasa, visiwa vingi vina changamoto ya  ongezeko la idadi ya watu ambalo haliendani  na  mahitaji ya matumizi ya ardhi, hali ambayo inawafanya baadhi ya wananchi waanzishe makaazi na shughuli zao za maendeleo katika maeneo yaliyokuwa hayakutengwa na yanakaliwa kinyume na sheria.  Kwa hivyo, naamini kwamba masuala ya aina hii yatazingatiwa na kuwekewa mikakati madhubuti zaidi ya kisera na kisheria kwa ajili ya kuzitatua changamoto zilizojitokeza, ili hatimae tuweze kuwanusuru wananchi kutokana na maafa  yanayoweza kutokea.

Ndugu Washiriki,
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikipanga na kutekeleza mikakati mbali mbali  ya kukabiliana na maafa.  Serikali iliandaa Sera  ya  Kukabiliana na Maafa ya mwaka 2011, na baadae ilitunga  Sheria ya Kukabiliana na Maafa Nam 1 ya mwaka 2015 ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa Kamisheni ya Kukabliana na Maafa ya Zanzibar.  Vile vile, Serikali imeandaa  Mkakati wa Mawasiliano Wakati wa Maafa na Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa katika ngazi ya Kitaifa na  Wilaya.  Sambamba na juhudi hizo, Serikali  imeanzisha  kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ‘Emergency Operation and Communication Centre’ kilichopo eneo la Maruhubi Unguja. Vile vile, juhudi kubwa  za  kutoa elimu zinaendelea kufanywa,  ili kuwapa wananchi uwezo mkubwa wa  kujiandaa na kukabiliana na maafa. Elimu hio inatolewa  kupitia Vyombo vya Habari vya Serikali na vya Sekta Binafsi, mikutano ya kijamii, semina na makongamano mbali mbali. Kadhalika, elimu imekuwa ikitolewa juu ya tahadhari za mapema kwa majanga mbalimbali yanayoweza kuikumba jamii yetu, ikiwemo athari za mvua kubwa na upepo mkali. Kadhalika, Serikali imeimarisha shuguhuli za kufanya ukaguzi katika maeneo tafauti kwa ajili ya kuangalia mipango na taratibu za kukabiliana na maafa. Maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na vyombo vya usafiri, hoteli, majengo ya umma, vituo vya kuuzia mafuta na gesi na maeneo yenye kukumbwa na mafuriko ya mara kwa  mara.
Ndugu Washiriki,
Shughuli za uvuvi na usafiri wa baharini ni sehemu muhimu ya maisha ya wananchi wa Zanzibar, kama ilivyo katika visiwa vyengine.  Shughuli hizi baadhi ya wakati huambatana na ajali mbali mbali. Miongoni mwa ajali kubwa za meli zilizotokea Zanzibar na zilizoacha athari isiyosahaulika kwa wananchi wa Zanzibar ni ajali ya kuzama meli ya “MV Spice Islander” katika eneo la Nungwi - Zanzibar mwaka 2011, na ajali ya kuzama kwa meli  “MV Skagit” mwaka 2012. Baada ya maafa haya makubwa,Serikali iliongeza nguvu kubwa za kujikinga na ajali za baharini.

Katika hatua za kujikinga na majanga kama hayo, Serikali iliandaa mikakati maalum ya kuimarisha huduma za usafiri wa baharini  pamoja na kuishajiisha sekta binafsi, ili nayo iwekeze kwa kununua  vyombo vya baharini. Serikali imenunua meli mbili za kisasa, Mv. Mapinduzi II kwa ajili ya kuimarisha usafirishaji wa abiria na MT Ukombozi II kwa ajili ya usafirishaji wa mafuta. Wawekezaji wazalendo  nao wamehamasika katika kuziunga mkono jitihada za Serikali za kujilinda na kupunguza matukio ya maafa baharini, kwa kununua boti za  abiria za mwendo kasi za kisasa  pamoja na meli za abiria na Mizigo, ili zitumike pamoja na zile zilizokuwepo awali.  Hivi sasa, tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha usafiri wa baharini, jambo ambalo limewapelekea watalii na wageni wengi wanaopenda kuja Zanzibar kutoka Tanzania Bara kutumia usafiri wa baharini  badala ya  usafiri wa  anga. Naamini kwamba baadhi yenu mmetumia usafiri wa  baharini wakati mliposafiri kuja kwenye mkutano huu, na mmejionea wenyewe ubora wa vyombo mlivyosafiria.

Ndugu Washiriki,
Pamoja na ununuzi wa vyombo vya kisasa vya usafirishaji wa abiria, mizigo na mafuta, Serikali imejenga vituo vitatu vya uokozi (rescue centers) vinavyosimamiwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), katika eneo la Nungwi na Kibweni kwa Unguja pamoja na Mkoani kwa upande wa Pemba, ili tuwe na uwezo mkubwa zaidi wa  kutoa huduma za uokozi na kwa haraka, pale ambapo huduma hizo zitahitajika. Vile vile, Serikali imenunua mitambo mbali mbali na  ndege zisizo na rubani (drones), ili kuweza kujua hali ya usalama wa  meli na vyombo vya baharini  vilivyopo  au vinavyopita  katika eneo la Zanzibar.

Zaidi ya hayo, Serikali imenunua  boti mbili (2) za kisasa;  moja ya uokozi yenye  uwezo wa kuokoa watu wapatao mia nne (400) kwa wakati mmoja na nyengine ya  kuzimia moto baharini, ambayo hivi sasa  inasimamiwa na Kikosi chetu cha Zimamoto na Uokozi, kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto baharini.

Ndugu Washiriki,
Katika kukabiliana na maafa yanayotokana na mvua pamoja na mafuriko, hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inaendelea na  ujenzi wa nyumba za wananchi walioathiriwa na Mvua za Masika za mwaka 2017, katika maeneo ya Nungwi  kwa Unguja na Tumbe kisiwani Pemba, ambapo jumla ya nyumba 30, msikiti, skuli, kituo cha afya na soko vitajengwa katika maeneo hayo.

Serikali imekuwa ikitekeleza Mradi wa Kuendeleza Huduma Mjini (ZUSP) unaotekelezwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia wenye jumla ya Dola za Marekani Milioni 93, ambapo mambo kadhaa yanatekelezwa pamoja na kuondoa tatizo la mafuruiko katika maeneo yote yanayokumbwa na maafa hayo katika  mji wa Zanzibar.  Kwa hivyo,  utekelezaji wa mradi huu  umejumuisha ujenzi wa misingi mine mikubwa ya kuondoa maji ya mvua na kuyapeleka baharini kutoka kwenye maeneo yenye kukumbwa na mafuriko wakati wa mvua kubwa.  Hivi sasa, utekelezaji wa mradi huo umeshafikia zaidi ya asilimia 90 na tunatarajia maji hayatotuama tena katika maeneo hayo na mafuriko hayatotokea.
Ndugu Washiriki,
Mafanikio haya ni matunda ya jitihada za Serikali na wananchi ambazo zinaungwa mkono na Taasisi na Jumuiya mbali mbali za Kimataifa. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itaendelea kushirikiana na   SADC katika utekelezaji wa mipango mbali mbali yenye lengo la kuimairsha namna ya kujikinga na maafa katika nchi wanachama. Imani ya wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ni kwamba, tutaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa SADC katika masuala  muhimu ya maafa, ili tuwe na mfumo endelevu wa kukabiliana na maafa katika ngazi zote.

Tuna jukumu la kuendelea kushirikiana kati ya Serikali zetu, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa, Taasisi za Utafiti, Sekta Binafsi, Taasisi za Kidini, Taasisi za Fedha na  Mashirika yasiyo ya Serikali, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari katika suala hili. Tukifanya hivyo, itakuwa tumeitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mkutano huu isemayo:  “Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.”  Vile vile tuhakikishe kwamba tunaandaa na tunautekeleza mfumo mzuri  wa kutoa mafunzo na kubadilishana uzoefu baina ya  wataalamu wa nchi wanachama wa SADC , katika masuala mbali mbali yanayohusu maafa.

Naamini kwamba  mkutano huu utapitisha maazimio  ambayo yatatuongoza katika juhudi zilizopo za kuimarisha ushirikiano wetu katika masuala ya maafa pamoja na kuongeza ushawishi kwa nchi  wanachama  kuwekeza  zaidi kwa ajili  kuimarisha  mifumo ya utoaji wa  tahadhari, kuimarisha  teknolojia ya kuufahamu mfumo wa hali ya hewa,  kuimarisha vituo na vifaa vya uokozi, kutenga maeneo ya kukimbilia na kujihami wakati wa dharura katika nchi zote wanachama na kuwa na utaratibu wa kushirikiana kwa wataalamu, vifaa pamoja na misaada ya kibinadamu.

Ndugu Washiriki,
Kabla sijamalizia hotuba yangu, nataka nikujuuilisheni ndugu zangu, wajumbe wa Mkutano huu, kwamba tunaandaa mpango wa mafunzo  kwa ajili ya walimu wa kwenda kusomesha Kiswahili katika mataifa yenu, tukitilia maanani kwamba tayari lugha ya Kiswahili ilichaguliwa kuwa miongoni mwa lugha za mawasiliano katika mikutano ya Jumuia ya Nchi za SADC. Kwa hivyo, nakuhamasisheni ndugu wajumbe wa Mkutano, muwalete walimu wenu, ili  waje wajifunze Kiswahili hapa Zanzibar.

 Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kinaendesha mafunzo ya Kiswahili kuanzia elimu ya Cheti hadi Shahada ya Uzamivu (Ph.D).

Namalizia hotuba yangu kwa kukutakieni  mshiriki vizuri  katika mkutano huu, ili kwa pamoja tuweze kuyafikia malengo yaliyopangwa. Kwa mara nyengine, natoa shukurani kwa Kamati ya Maandalizi  ya Mkutano huu kwa kuamua  kuufanya Mkutano huu hapa Zanzibar na kunialika niwe Mgeni rasmi. Tunakukaribisheni nyote Zanzibar  wakati wote  kwa moyo mkunjufu.  Nnakukumbusheni msikose kuitumia fursa ya  kushiriki katika mkutano huu bila ya kutembelea vivutio vyetu vya utalii, pamoja na Mji Mkongwe, ili mzidi kuifahamu historia ya Zanzibar na watu wake. Karibuni sana.
Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kuiongoza vyema nchi yetu kwa mafanikio makubwa na kwa sababu alikabidhiwa rasmi uongozi na Jumuiya hii wa kuwa Mwenyekiti wa SADC, nampongeza kwa kaanza vizuri, sina shaka na mafanikio tutakayoyapata katika uongozi wake, Rais Magufuli ni muadilifu katika kuoingoza nchi hii kwani ndani ya miaka minne ya uongozi wake Tanzania imeweza kupata mafanikio makubwa na kujijengea sifa kubwa.
Baada ya kusema hayo, natamka kwamba Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana ya  Menejimenti ya Maafa umefunguliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top