Na Mwandishi
Wetu, Zanzibar
LICHA ya uwepo wa malalamiko kwa baadhi
ya wananchi wanaodai kukosa kuandikishwa katika daftari la wapiga kura, kwa
sababu mbali mbali, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema tathmini kamili ya
zoezi zima inatarajiwa kufanyika baada ya zoezi hilo kukamilika.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alitoa kauli hiyo katika
muendelezo wa zoezi hilo linaloendelea huko kaskazini Unguja kwa Wilaya ya
Kaskazini ‘’A’ na ‘B’.
Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi
hilo tume itafanya tathmini ili kuangalia kwa namna ambavyo itaweza kusaidia
kuzitatua changamoto za Wananchi ambao wamekosa fursa ya kuandikishwa katika
Daftari kutokana na sababu mbali mbali ikiwamo ya kukosa Vitambulisho vya
Mzanzibar Mkaazi.
Alisema kutokana na uwepo wa malalamiko
hayo uongozi wa tume hufanya ziara katika vituo kwa kupata tathmini ya awali
ili kujua mafanikio na changamoto juu ya utaratibu wa uandikishaji na uhakiki
wa taarifa za wapiga kura unavyoendelea.
Kwa upande wa mwanasheria
mkuu wa zamani wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary alisema zoezi la Uandikishaji katika Daftari la kudumu la Mpiga kura, linashangaza
sana kuona Tume inakataa kuwaadikisha wananchi ambao hawajapatiwa kitambulisho
kipya cha Mzanzibar mkaazi, lakini vitambulisho vya zamani wanavyo.
Alisema kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi, huku akiweka wazi
kwamba ACT wataendelea kudai haki ya wananchi wake, ili kuona kila mwananchi
anaandikishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo Abubakar alidai kuwa watendaji wa ofisi ya Vitambulisho vya
Mzanzibar Mkaazi kwa kushirikiana na tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) hawana nia
njema na ndio maana hadi leo hii wananchi walio wengi hawana vitambulisho.
Hata hivyo kwa upande wa Mkurugenzi Wakala wa Matukio ya Kijamii
Zanzibar, Dk Hussein Khamis Shabani hivi karibuni alisema ukosefu wa
vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi kwa baadhi ya wananchi kunatokana changamoto
za kukosewa kwa baadhi ya taarifa za wananchi hao na si vyenginevyo.
Alisema waliokosa vitambulisho hivyo kwa awamu ya kwanza wasiwe na
hofu na kwamba kila mtu aliekidhi vigenzo vya kisheria vya vya kupatiwa
kitambulisho hicho ajue atapatiwa bila ya usumbufu wowote.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit
Idarous Faina alisema wao kama tume ya uchaguzi (ZEC) hawahusiki na utoaji wa
vitambulisho na kwamba kinachowahusu wao ni uandikishaji wa piga kura wapya na
uhakiki kwa wale wote wa zamani.
Faina
alisema alisema
Tume ya Uchaguzi itamuandikisha kila mwananchi aliyetimiza sifa za kuandikishwa
katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya
Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018 ili kuweza kupiga kura katika Uchaaguzi Mkuu wa
2020.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment