Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wazee wanasiowapeleka shule watoto wenye mahitaji maalum (wenye ulemavu) kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa   sheria ya elimu visiwani hapa.

Imesema kila mtoto aliyetimiza umri wa miaka minne ana haki ya kupatiwa elimu kuanzia mandalizi hadi Secondari bila ya kujali hali yake ya kifedha au mwenye ulemamavu “mahitaji maalum”.

 Waziri wa elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alibainisha hayo katika Mahafali ya Mafunzo ya Ualimu wa Maandalizi ngazi ya cheti ya Chuo Cha Madrasa Early Childhood Training College yaliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Habari Kilimani Unguja.

Alisema lengo la serikali kufuta michango ya elimu kuanzia ngazi ya mandalizi hadi Secondary ni kuona kila mtoto anapatiwa haki ya kupata elimu, bila ya kujali hali yake ya kimaisha, akibainisha kuwa kutokana na hali hiyo ni lazima kwa watoto wote kupelekwa shule umri unapotimia.

Hata hivyo Waziri Pembe alisema uwepo wa walimu wenye taaluma ya Maandalizi ni mkakati wa Wizara wa kuhakikisha watoto wanapata Msingi mzuri wa Elimu,kwani elimu zote zinahitaji Msingi kwanzia Elimu ya Maandalizi.

Alisema kuwepo kwa walimu wenye ujuzi wa kusomesha na kusaidia watoto kutasaidia taifa kuzalisha wasomi na wataalam wa fani mbalimbali.

Alisema mpango Mkuu wa Elimu Zanzibar 2017/2018 mpaka 2020/2022 unaonesha mahitaji ya walimu wa maandalizi wenye sifa ili kuendana na kasi ya uandikishaji wa watoto katika Skuli za Serikali na binafsi.

Aidha, Serikali imeondosha ada kwa Wanafunzi wa Maandalizi na Msingi katika Skuli zote za Serikali kwa nia ya kutoa fursa kwa Wananchi kupata Elimu na kuweza kuzalisha wataalam wazalendo.

Waziri Pembe alisem Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha mazingira mazuri ya kusomeshea kwa kukamilisha madarasa na majengo mapya, akisisitiza kuwa Wizara yake inaendelea kuupitia mtaala wa Elimu ya Maandalizi na Msingi ili Wanafunzi waandaliwe kwa mujibu wa mahitaji ya nchi.

Hata hivyo amewasisitiza Wahitimu wa Mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia ujuzi na maarifa waliyopatiwa katika mafunzo ili kuwajenga watoto kitaaluma zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Madrasa Early Childhood Training College, Khamis Abdalla Said amesema Walimu waliosoma katika chuo hicho anahakikisha wanapata ujuzi wa kuwaandaa watoto wa Maandalizi kujua kusoma na kuandika, pia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kwa mashirikiano mazuri na sekta Binafsi katika kuleta maendeleo ya kuaji katika sekta ya Elimu nchini.

Kwa upande wake mrajisi wa Elimu Zanzibar, Siajabu Suleiman Pandu amewataka wazazi kuwasomesha watoto wao katika Vyuo vilivyopata usajili wa Mamlaka za Kielimu ili kuepuka kupoteza gharama na muda katika Vyuo ambavyo vimekosa usajili serikalini.

Nao Wanafunzi katika risala yao wameiomba Wizara ya Elimu Zanzibar kupatiwa nafasi za ajira kwa wanafunzi wanaosoma Chuo hicho hasa kwa wale Walimu wanaojitolea Katika Skuli mbalimbali za Mjini na vijijini.

Katika mahafali hiyo ya tatu Jumla ya Wanafunzi 66 wamehitimu wakiwemo Wanaume watatu.

Imeandikwa na Haji M. Mohd

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top