Zanzibar
ni miongoni mwa nchi iliyojaaliwa neema ya bahari nzuri na yenye
kuvutia ambayo wananchi wake pamoja na serikali kwa ujumla wamekuwa
wakiitumia katika shughuli mbali mbali za kijamii, kiuchumi na
maendeleo.
Miongoni mwa
shughuli ambazo hutumika kupitia uwepo wa bahari visiwani hapa ni pamoja
na uvuvi, kilimo cha mwani, Utalii pamoja na shughuli nyengine mbali
mbali zenye kuingiza kipato kwa jamii na taifa.
Licha
ya habari kutumika kwa matumizi mbali mbali, lakini matumizi makuu ya
bahari visiwani hapa ni uvuvi ambao hutoa fursa kubwa hasa kwa wananchi
wanaoishi maeneo ya karibu na habari au wakati mwengine hata waishio
maeneo ya mbali.
Hii ni
moja ya fursa ambayo imekuwa ichangamkiwa kwa kasi hasa na vijana
wanaoishi pembezoni mwa bahari, kutokana na utendeaji kazi wake
hauhitaji elimu ya shule, chuo au utaalaam ambao upatikanaji wake huwa
mgumu kwa wanyonge.
Ni
vijana wengi wamekuwa wakinufaika na matumizi ya bahari ambapo baadhi
yao kupitia kazi ya uvuvi hawatamani hata kazi nyengine, kutokana na
uingizaji wa kipato chake huwa ni kikubwa ukilinganisha na baadhi ya
kazi nyengine za kawaiada.
Hakuna
asiyefahamu kwamba kazi ya uvuvi imegawika katika maeneo mbali mbali,
wapo wavuvi, madalali wa kuuza samaki, wanunuzi pamoja na wahudumu wa
mwisho ambao ni waparaji samaki baada ya wanunuzi kununua.
Kwa
kuwa kazi ya uparaji wa samaki kuonekana ni kazi ya mwisho kabisa
katika sekta ya uvuvi, imeonekana ni jambo la kawaida katika maeneo
mbali mbali visiwani hapa watoto walio chini ya miaka 18, ndio wahusika
wakuu wa uparaji wa samaki.
Ni
maeneo mengi hasa katika masoko ya samaki vijijini watoto ni wahusika
wakuu wa kazi hiyo, ikidaiwa kuwa hali hiyo husababishwa na kipato cha
uparaji wa samaki kuwa ni kidogo, hivyo kazi hiyo mara nyingi huwaachiwa
watoto .
Baadhi ya
watoto hufanya kazi hiyo huku wazazi au walezi wao wakitambua au wakati
mwengine wao ndio huwa wasimamizi wakuu wa kuona watoto wao wanapata
kazi nyingi ili kupusha suala la kuombwa pesa ovyo na vijana wao hao.
Licha
ya wazazi hao kuona wanachofanya kuwa ni sahihi kwa maslahi yao dhidi
ya watoto hao, lakini ukweli ni kwamba kufanya hivyo ni kuwadumaza
watoto kiakili pamoja na kuwaandaliwa maisha mabaya hapo baadae, kwani
baadhi ya watoto hao shule wamekatisha.
Ni
mara nyingi sana tumekuwa tukisikia malalamiko ya walimu wa shule hasa
kwa shule zilizopo karibu na bahari, wakidai kuwa utoro pamoja na
ukataji wa masomo kwa watoto wa maeneo hayo yamekuwa ni mambo ya
kawaida.
Huku wazazi wao
wakiwa hawana hata wasi wasi juu ya watoto, licha ya juhudi kubwa
kuchukuliwa na walimu kuitisha vikao mara kwa mara ili kujadili
mustakabali mzuri juu ya utoaji wa elimu kwa watoto.
Ifahamike
kwamba licha ya wazazi kuona kufanya hivyo ni kuwapenda watoto au
kuwapa mbinu za kutafuta pesa mapema, lakini njia hiyo ni kuwapotosha
watoto na kuwaandalia mazingira mabaya katika maisha yao ya baadae.
Umefika
wakati sasa kwa wazazi, taasisi mbali mbali za wanaharakati pamoja na
serikali kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja katika kulifanyia kazi suala
la watoto kutoshirikia kazi ya uparaji wa samaki, ili kuona watoto hao
wanaandaliwa vyema ili kuja kuwa viongozi wazuri wa familia, au serikali
hapo baadae.
Licha ya
taasisi mbali mbali kikiwamo cha Waandishi wa habari za Maendeleo
Zanzibar (Wahamaza) Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto (Unicef)
kufanya kazi kuwa ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa elimu na malezi bora
kwa watoto, lakini bado wazazi wana haki kubwa ya kuona watoto wao
wanaishi katika mazingira bora.
Tunaamini
hilo linawezekana pindi kila mmoja akatambua umuhimu wa kuwatunza na
kuwalea watoto katika makuzi bora hasa ya kielimu ni jukumu la kila
mmoja, ili baadae kuja kufurahia matunda ya kuwa na wataalam wenye sifa
nzuri kutoka ndani ya nchi badala ya kuwa na wataala kutoka nje ya nchi.
Imeandiliwa na Haji M. Mohd, chini ya ufadhili wa UNICEF
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment