Wakala wa Chakula
na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeanza ukaguzi wa wauza maziwa wasiofuata utaratibu
unaokubaliwa ikiwemo sehemu zisizo rasmi ili kulinda afya za wananchi.
Mkurugenzi Idara
ya Udhibiti Usalama wa Chakula wa ZFDA Dk. Khamis Ali Omar alisema ukaguzi umefanyika
baada ya kutoa elimu na matangazo kwa wauza maziwa kuacha kutumia chupa na
madumu ya plastiki na katika maeneo yasiyo rasmi.
Alisema chupa
na madumu ya plastiki baada ya kutolewa maziwa hayawezi kusafika na hubakisha
chembe chembe za maziwa wakati wa kukosha ambazo baada ya muda huoza.
Dk. Khamis
alisema zoezi hilo litakuwa endelevu na amewataka wauzaji wa maziwa kufuta
maelekezo yanayotolewa na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ili kujiepusha na
gharama zisizo za lazima.
Alisema chupa
na madumu ya plastiki ambayo yamekuwa yakitumiwa na wauza maziwa hayapo salama na
yanaweza kusababisha maradhi ya kuambukiza ikiwemo kifuakikuu.
Aliwashauri wauzaji
wa maziwa kuwa na maeneo maalumu ya kuuza bidhaa hiyo kwa kutumia chupa za vigae
zilizopunguzwa mwangaza na kutumia keni za aluminiam kubebea maziwa.
Muuza maziwa wa eneo la Amani Haroun Abdalla alikiri
kuwa ZFDA walitoa elimu kuhusu madhara
ya kutumia chupa na madumu ya plastiki lakini muda waliopewa kujitaarisha
kutumia chupa za vigae na keni za alluminiam ni mfupi.
Alisema bei
ya keni moja ya kubebea maziwa inagharimu zaidi ya shilingi laki mbili kiwango
ambacho wauzaji wadogo waliowengi wengi hawawezi kumudu kununua kwa kipindi
kifupi.
Muuzaji mwengine
Ali Muhamed alisema tatizo kubwa liliopo Zanzibar hakuna kiwanda kinachozalisha
chupa za vigae zinazotakiwa kutumika kwa ajili ya kuuzia maziwa.
Katika
ukaguzi huo wafanyakazi wa ZFDA waliharibu lita kadhaa za maziwa waliyoyakuta yakiuzwa
katika sehemu zisizo rasmi na kutumia chupa na madumu ya plastiki.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment