Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Mitawi akimlisha kipande cha Keki Balozi Seif kama ishara ya kumpongeza kwa kutimia Miaka 78 |
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi amewaasa Watumishi wachanga na wale wanaoendelea na Majukumu yao kwa sasa katika Taasisi za Umma na zile
Binafsi kuzingatia kwa kina suala la Utii kwenye utekelezaji wa Kazi za kuhudumia
Jamii mahali popote pale.
Alisema Utii ndio dhana nzito, sahihi na
inayobeba ngao kubwa kwa Mtumishi ye yote na matokeo yake hujikuta akipata
fursa nyingi zinazomuwezesha kuheshimika sambamba na kupanda daraja katika
maeneo yake ya Kazi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa wasia huo
kufuatia Uongozi na Wafanyakazi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kumfanyia tafrija ndogo ya kushtukiza baada ya kutimiza Miaka
78 ya Siku yake ya kuzaliwa ifikapo Tarehe 23 Febuari ya kila Mwaka.
Alisema yeye akiwa miongoni mwa Watumishi wa
umri mrefu wa kazi usiopungua Miaka Sitini katika nafasi mbali mbali za
Utumishi wa Umma ameshuhudia mambo mengi katika mafanikio ya huduma za Kijamii
yaliyobebwa na dhana ya Utii uliotukuka.
“ Huwezi kupata mafanikio yoyote katika
Taasisi iwe za Umma, Binafsi na hata Familia kama hutakuwa na Utii kwa wale
waliokuzunguuka muda wote katika matendo yako ya kila Siku”. Alisema Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif
alieleza kwamba katika umri wake hata akiwa nje ya Utumushi wa Umma
ataendelea kutoa busara zake kwa wale wote watakaokuwa tayari kuchota busara
hizo muhimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliupongeza Uongozi pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi
chote cha kuiongoza Wizara hiyo ndani ya Muda wa Miaka Tisa na Nusu.
Alisema Ushirikiano huo kwa kiasi kikubwa
ndio ulioleta mafanikio makubwa ndani ya Wizara hiyo iliyo inayosimamia
Shughuili za Serikali yanayoshuhudiwa na Wananchi walio wengi Mjini na
Vijijini.
Akitoa shukrani kwa Niaba ya Uongozi na
Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Kaimu Katibu Mkuu wa
Ofisi hiyo Nd. Abdullah Hassan Mitawi alisema Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi
ni Tanuri lenye mambo mengi yanayoweza kutumiwa na Watendaji wachanga.
Kaimu Katibu Mkuu Mitawi alisema tanuri hilo
lililojaa busara, uzoefu pamoja na hekina
za takriban Miaka Sitini litakuwa chachu ya kuchotwa na Viongozi na
Watendaji wachanga katika Utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya
kuwatumikia Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi alizaliwa Mnamo Tarehe 23 Febuari Mwaka 1942 katika Kijiji cha
Mgambo Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja na kupata Elimu za Dini
na Dunia kama walivyo Watoto wote wa Ukanda wa Mwambao.
Balozi Seif alipata Mafunzo ya Ualimu Beit El
Ras na kuanza Kazi ya Kufundisha katika Skuli ya Kinyasini iliyo jirani na
Kijiji chake ambapo jitihada zake zilimuwezesha kuteuliwa kuhamia Wizara ya
Mambo ya Nje ya Tanzania akiwa Afisa wa Kawaida.
Aliendelea na wadhifa huo uliobadilika kila
kukicha kutokana na Utii wake katika kazi iliyompandisha daraja na kuwa Balozi
kamili wa kuiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi kirefu
na Mataifa mbali mbali Duniani.
Balozi Seif Ali Iddi alistaafu Kazi kwa
mujibu wa Utumishi wa Umma na kuamua kuingia katika ulingo wa Kisiasa
uliomuewesha kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi {CCM} kwa
Upande wa Zanzibar.
Ulingo huo wa Kisiasa ulimfungulia njia na
kuchaguliwa na Wananchi kuwa Mbunge wa Jimbo lililokuwa la Kitope kwa Tiketi ya
Chama cha Mapinduzi {CCM} katika Vipindi Viwili na kupata nafasi ya kuteuliwa
kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Tanzania Miaka Mitano ya awali.
Kutokana na Utii aliokuwa nao Balozi
Seif wakati bado akiendelea kuwa Mbunge
wa Kitope Awamu ya Pili ulimshawishi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kumteuwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar.
Baadae aliamua kugombea nafasi ya Ujumbe wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar nafasi iliyompa fursa ya Kuteuliwa kuwa Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ndani ya kipindi cha Miaka na Nusu sasa.
Balozi Seif Ali Iddi wakati akiyafungua Mafunzo ya Vijana
katika Chuo cha Ujasiri Amali cha Wadi ya Mahonda hapo kwenye Tawi la CCM
Kitope “B” Mnamo Tarehe 15 Oktoba Mwaka 2018 alitoa kauli ya kutogombea tena
nafasi ye yote ameshatangaza Rasmi kujipumzisha na shughuli za Kisiasa
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment