KUANZISHWA kwa utafiti wa mradi wa nishati rafiki na matumizi bora ya nishati mbadala ni njia moja ya kuiwezesha Zanzibar kuwa na vyanzo vyake vya ndani vya nishati.

Hayo yalielezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Tahir Mohammed, wakati akifungua mafunzo elekezi juu ya midahalo kupitia klabu za mazingira kwa skuli za sekondari kuhusu Zanzibar kuwa na vyanzo vyake vya nishati, yaliyofanyika ukumbi wa elimu mbadala Rahaleo.

Alisema mradi huo umejihusisha na utafiti wa kuangalia uwezekano wa kuzalisha umeme kutokana vyanzo vya nishati ya upepo na jua.

Alisema, lengo la mafunzo hayo ni kutoa ufahamu kuhusu nishati mbadala kwa Zanzibar na kupata ufumbuzi wa kuwa na nishati endelevu ambayo itahifadhi mazingira.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaisaidia serikali kuweka mazingira wezeshi kisera na kisheria kwa ajili ya kuwezesha nishati rafiki na kutoa elimu ya ufahamu kwa wananchi na sekta binafsi kuhusu nishati mbadala.

Hata hivyo, alisema ikumbukwe kuwa Tanzania Bara kwa muda mrefu imekua ikizalisha nishati ya umeme kutokana na maporomoko ya maji huku vyanzo vyengine ni makaa ya mawe na gesi inayopatikana mkoani Mtwara.

Alisema Zanzibar inakosa chanzo muhimu cha nishati ya maporomoko ya maji na badala yake inategemea nishati ya umeme kutoka Tanzania bara.

Alibainisha kuwa, kuharibika kwa mazingira huathiri maisha ya viumbe vvyengine kama binaadamu, wanayama na hata mimea hivyo ni vyema nishati hizo ziwe rafiki na mazingira na vitu vilivyomo.

Aliwasisitiza wanafunzi waliopata fursa hiyo kuitumia vizuri ili kuielimisha jamii na kuwa chachu ya kueneza na kuleta mabadiliko katika jamii zao.

Omar Saleh Mohammed, Msaidizi Mkuu wa mradi wa nishati rafiki kutoka idara ya nishati na madini,  alisema wanaendelea kufanya utafiti wa nishati mbadala na kuangalia jinsi Zanzibar inavyoweza kupata vyanzo vya kuzalisha umeme.

Alisema, hivi sasa wamejikita zaidi katika vyanzo vya jua na upepo na utafiti uliofanywa mwaka 2012 ulibainisha vyanzo vingi lakini vilivyopata nafasi ya kwanza ni jua na upepo.
chanzo, zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top