UAMUZI wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa kuzuia uingiaji wa nguo za mitumba ifikapo mwaka 2019, umegonga mwamba baada ya kujitokeza mgogoro baina ya nchi za EAC na Marekani, ambayo ndio mzalishaji mkubwa wa nguo hizo.
Serikali za nchi wanachama wa jumuiya hiyo ziliweka azimio hilo, ikiwa ni hatua ya kutaka kuinua uzalishaji wa ndani wa nguo.
Nchi wanachama wa EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Congo, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.
Akizungumza na Zanzibar Leo, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, alisema nchi hizo zimeshindwa kutekeleza makubaliano hayo, baada ya Marekani kutoa kitisho cha kuwabana katika soko la AGOA.
AGOA ni mkataba unaotoa haki ya kutotozwa ushuru kwa karibu bidhaa zote zinazoingizwa katika soko la Marekani, kutoka nchi walengwa ambazo ni pamoka na nchi za Afrika Mashariki.
Alisema kitisho hicho kilizifanya nchi hizo kufanya kikao cha pamoja ambapo Kenya iliamua kujitoa katika msimamo huo na kutangaza kuwa itaendelea kuingiza nguzo za mitumba, huku Tanzania, Rwanda na Uganda zilikubaliana kuendelea na azimio hilo.
Alisema katika kulifanyia kazi suala hilo walichukua hatua ya kupeleka ujumbe nchini Marekani na kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo, ambapo walikubaliana kutumia utaratibu mwengine.
“Tulituma ujumbe kwenda kuzungumza na serikali ya Marekani na wakakubaliana kuwa na utaratibu mwengine ambao utawasilishwa katika kikao cha mawaziri wa Afrika Mashariki,” alisema.
Alisema kikao hicho nacho kilishindwa kukubaliana na sasa suala hilo linatarajiwa kufikishwa katika kikao cha marais ambacho kitafanyika nchini Uganda baadae mwezi huu.
Hata hivyo, alisema kuhusu uingizaji wa nguo za ndani bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuzuia uingizaji kwa sababu zina madhara kiafya.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment