Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Baadhi ya wananchi waliokosa waliokosa kufanyiwa uhakikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa madai ya kutokuwa na kitambulisho kipya cha mzanzibar mkaazi wametinga Mahakamani ili kudai haki yao kisheria.

Wananchi ni kutoka kisiwani Pemba akiwemo Mohd Ali Salim pamoja na wenzake watatu, ambao wote kwa pamoja wamefikia maamuzi hayo baada ya kuona wana haki ya kufanya hivyo, juu ya kudai haki yao kisheria kupitia vyombo vya sheria.

Mwanasheria wa wananchi hao, Omar Said Shaaban alisema kuwa tayari wameshapeleka maombi ya wateja wake Mahakani ya kuomba ruhusa ya kupatiwa kibali cha kufungua Jalada la kutaka kufanyike mapitio ya maamuzi ya Tume ya Uchaguzi kwa kuagiza watu watakaoandikishwa ni wale wenye vitambulisho vipya vilivyo hakikiwa tu.

Alisema kwa mujibu wa sheria ili kufungua jalada la kufanyika mapitio kwa madai kama hayo ni lazima Mahakama itoe kibali kwa wale wanaomba kufungua jalada la kufanyika mapitio.

Alisema kupitia maombi hayo tayari wameshapewa siku ya tarehe 26 February mwaka huu, kuwa ni siku ya kusikilizwa ombi lao kupitia Jaji Aziza Idd Suweid wa Mahakama kuu, huku akibainisha kuwa na matumaini makubwa ya kwamba wateja wao hao watapata kibali hicho kutokana na ombi lao kuwa la msingi.

“Pindi wateja wetu watakapokosa kibali cha kufungua jalada la kuomba kufanyika kwa mapitio hayo, tutaangalia njia nyengine za kisheria ili kuona haki wanazodai zinapatikana, ila kwa sasa hatuwezi kusema zaidi kutokana na Mahakama ndio yenye maamuzi zaidi juu ya hilo”alisema.



Kwa upande wa Mkurugenzi Wakala wa Matukio ya Kijamii Zanzibar, Dk Hussein Khamis Shabani akizungumzia kadhia hiyo hivi karibuni alisema ukosefu wa vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi kwa baadhi ya wananchi kunatokana changamoto za kukosewa kwa baadhi ya taarifa za wananchi hao na si vyenginevyo.  

Alisema waliokosa vitambulisho hivyo kwa awamu ya kwanza wasiwe na hofu na kwamba kila mtu aliekidhi vigenzo vya kisheria vya vya kupatiwa kitambulisho hicho ajue atapatiwa bila ya usumbufu wowote.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa uchaguzi  Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina alisema wao kama tume ya uchaguzi (ZEC) hawahusiki na utoaji wa vitambulisho na kwamba kinachowahusu wao ni uandikishaji wa piga kura wapya na uhakiki kwa wale wote wa zamani.

Faina alisema Tume ya Uchaguzi itamuandikisha kila mwananchi aliyetimiza sifa za kuandikishwa katika daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018 ili kuweza kupiga kura katika Uchaaguzi Mkuu wa 2020.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top