RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kujidhatiti na kuwa na programu maalum ya mafunzo itakayowezesha kuwa na walimu wa kutosha wa masomo ya Sayansi, ili kuondokana na upungufu uliopo kwa walimu wa kada hiyo.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji ya mpango kazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba, kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Alisema ni vyema Wizara ikaandaa utaratibu wa muda mfupi utakaowawezesha wahitimu wa Sekondari waliofaulu vyema masomo ya Sayansi pamoja na wale wanaomaliza shahada katika vyuo vikuu nchini, kujiunga katika mafunzo hayo na hatimae kugaiwa katika skuli mbali mbali.
Alisema katika kipindi cha miaka 56 tangu Mapinduzi ya 1964, sio jambo jema kwa Zanzibar kubaki na tatizo la upungufu wa walimu wa Sayansi na kuendelea kutegemea misaada ya walimu kutoka nje ya nchi.
Alieleza kuwa Wizara hiyo ni ya kitaaluma na yenye watendaji weledi na wenye uzoefu, hivyo ni vyema wakajipanga ili kumaliza kabisa kadhia hiyo iliodumu kipindi mrefu.
Aidha, alishauri Wizara hiyo kuandaa na kutuma waraka maalum Serikalini juu ya azma ya kuwa na maktaba mpya ya kisasa itakayojikita katika matumizi ya mitandao.
Alisema kupitia sekta tofauti Zanzibar imekuwa ikianzisha majengo mbali mbali ya kisasa, hivyo ni muhimu pia kuwa na maktaba ya kisasa ili kuchochea maendeleo ya kielimu nchini.
Vile vile, aliishauri Wizara hiyo kutuma mapendekezo Serikalini kuangalia uwezekano wa kuwaajiri walimu 800 wanaofundisha katika vituo vya Tutu Unguja na Pemba, kwa kuzingatia uzito wa kazi hiyo yenye kuweka misingi bora ya kitaaluma kwa wanafunzi.
Rais Dk. Shein, alitaka Wizara hiyo kuangalia uwezekano wa kuwa na skuli mbili zaidi za Wanawake mikoani, kutoka miongoni mwa skuli tatu zinazoendelea kujengwa, ili kufanya jumla ya skuli za jinsia hiyo kufikia nne Unguja na Pemba.
Vile vile, alibainisha umuhimu wa kuwepo utaratibu maalum wa kuwafikia wananchi wasiojua kusoma na kuandika katika shehiya mbali mbali nchini, ikiwa ni hatua ya kuondokana kabisa na jamii isiyojuwa kusoma na kuandika.
Akigusia umuhimu wa kufanya tafiti kwa mustakbali mwema wa maendeleo ya elimu nchini, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kukaa na kufikiria namna ya kuwa na taasisi ya ‘elimu na utafiti’ na vipi itakavyofanya kazi.
Alipongeza hatua ya uongozi wa Wizara hiyo ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika skuli, kwa kigezo kuwa huchangia mabadiliko chanya, hivyo akataka juhudi hizo kuendelezwa kwa kuzingatia sheria, sera, kanuni na miongozo ya Wizara bila ya kuathiri imani za kidini.
“Ukaguzi ni jambo zuri sana, ubora wa elimu unakuja kutokana na ukaguzi”, alisema.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kurejesha vuguvugu la michezo skulini katika ngazi za msingi na Sekondari kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Alisema Serikali ilianzisha Idara ya michezo, ambapo pamoja na mambo mengine lengo lake ni kuchochea vuguvugu la michezo mbali mbali katika skuli Unguja na Pemba, hatua iliyoliletea sifa kubwa taifa.
Alisema katika miaka iliyopita kila skuli ilikuwa na walimu na vipindi maalum vya michezo na hivyo kuibuwa ushindani katika michezo tofauti, jambo alilobainisha hivi sasa limepotea.
Alisisitiza umuhimu wa kufufua ushindani wa kimichezo katika skuli, ukiwemo ule wa ‘Inter House competition’ kwa kuanzia.
Aidha, aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kufanya juhudi kubadili mitazamo na fikra ghasi za baadhi ya wazee kuwa michezo inaviza ufahamu na maendeleo ya wanafunzi , jambo alilobainisha sio sahihi kwa kigezo kuwa ‘elimu na michezo’ ni mambo yenye uwiano na yanayokwenda sambamba.
Nae; Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, aliupongeza uongozi na watendaji wa Wizara hiyo kwa maandalizi bora ya taarifa iliotumwa, sambamba na utekelezaji mzuri wa majukumu yao.
Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma, alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango wa elimu wa mwaka 2019/2020, hatua iliyokwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015-2020.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na upatikanaji mzuri wa fedha, ambapo hadi kufikia Disemba, 2019 Wizara ilifanikiwa kupata jumla ya shilingi 100,838,538/ (sawa na asilimia 82) ya makisio ya nusu mwaka.
Alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne 2019 katika daraja la kwanza, pili na la tatu.
Alisema katika kipindi hicho idadi ya watahiniwa waliofaulu daraja la kwanza walikuwa 299, ikilinganishwa na watahiniwa 185 waliofaulu katika mitihani ya 2018.
Aidha, alisema katika uimarishaji wa miundombinu, skuli tisa kati ya skuli 12 za ghorofa zinazojengwa zimekamilika na kufunguliwa katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza kuwa Wizara tayari imezipatia samani na vifaa vya maabara skuli zilizofunguliwa pamoja na vitabu vya masomo mbali mbali, vikiwemo vya maktaba za skuli.
Waziri Pembe aliyataja mafanikio mengine yaliopatikana katika kipindi hicho kuwa ni muendelezo wa ujenzi wa vituo 22 vya Ubunifu wa Sayansi Unguja na Pemba, vinavyotarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa bajeti.
“ Tumefanikiwa kuimarisha huduma za Dakhalia zote za Unguja na Pemba kwa kuzipatia usafiri dakhalia mbili kati yake na kusaidia gharama za chakula kwa wanafunzi wote wanaokaa dakhalia”, alisema.
Aidha, alieleza jumla ya seti 11,560 za vikalio vya wanafunzi watatu watatu wa madarasa ya msingi vilinunuliwa kutoka nchini China, ambapo hatua za kuvisafirisha zikiwa zinaendelea, huku awamu ya kwanza ya seti 2015 za vikalio hivyo kwa ajili ya wanafunzi 6,045 vikiwa tayari vimewasili katika Bandari ya Zanzibar.
Vile vile alisema katika kipindi hicho Skuli za Sekondari za Serikali zimeingiziwa fedha katika akaunti za skuli zao, jumla ya shilingi 2,114,608,500/ kwa ajili ya kufuta michango ya wazazi katika elimu.
Katika hatua nyengine, Waziri huyo alisema katika utekelezaji wa mpango huo changamoto mbali mbali zilijitokeza, ikiwemo uhaba wa vitabu vya elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha Pili, hususan kwa masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.
Alisema pia kulikuwa na changamoto katika uimarishaji wa miundombinu ya madarasa kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wanafunzi na kufikia kigezo cha wanafunzi 45 kwa darasa ngazi ya msingi na wanafunzi 40 kwa sekondari, na kubainisha kuwa hivi sasa wastani wa wanafunzi 81 husoma darasa moja katika ngazi ya elimu ya msingi na wanafunzi 62 ngazi ya sekondari.
Alisema tatizo jengine ni kuwepo uhaba wa wataalamu wa maabara, maktaba na ICT katika skuli pamoja na uhaba wa vifaa vya kufundishia somo la TEHAMA.
Wakati huo huo, Uongozi wa Shirika la Magazeti ya Serikali umetakiwa kupanua wigo wa soko kwa kusambaza magazeti ya Zanzibar leo, The Spoti na Zanzibar Mail katika maeneo mbali mbali ya mikoa ya Zanzibar ili yaweze kuwafikia kirahisi wananchi.
Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba, 2019/2020.
Alisema shirika hilo linaweza kupata mafanikio makubwa na kuongeza kiwango cha uchapishaji wa magazeti kutoka kopi 3,000 zinazochapishwa hivi sasa hadi kufikia kopi 5,000 kwa kuzisambaza katika vituo mbali mbali mikoani kwa kutumia vipando vya kawaida kama vile Bajaji.
Aidha, Dk. Shein amesisitiza umuhimu wa Wizara hiyo kusimamia, kuzienzi na kutunza nyaraka na kumbukumbu za serikali, kwa kuzingatia kuwa ndio uhai na utajiri wa Taifa.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahamoud Thabit Kombo alisema katika kipindi hicho Wizara ilifanikiwa kutekeleza miradi mbali mbali katika idara na taasisi zake, ikiwemo uimarishaji wa maeneo ya Kihistoria ya Mvuleni, Mwinyimkuu na Mkamandume, (awamu ya pili) yaliotengewa jumla ya shilingi 300,000,000/.
Alisema katika eneo la kihistoria la Mvuleni, kampuni ya KIN INVESTIMENT iinayoshughulikia ujenzi huo tayari imesafisha eneo lote la mradi pamoja na kujenga jengo jipya la kutolea huduma pamoja na vyoo vitakavyotumiwa na wageni watakaofika eneo hilo.
Aidha, alisema katika kipindi hicho Wizara ilipokea ujio wa ndege kadhaa, ikiwemo kutoka nchi za Russia, Uganda na Poland ambazo zimekuwa zikifanya safari za moja kwa moja kutoka nchini mwao hadi Zanzibar.
Vile vile alisema Wizara kupitia Wakala wa Uchapaji wa serikali imeanza kujenga jengo la ghorofa mbili linalotarajiwa kuwekwa mitambo mipya na ya kisasa, ukiwemo mtambo wa kuchapisha madaftari ya wanafunzi wa Serikali.
Mapema, akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahamoud Thabit Kombo alisema katika kipindi hicho Wizara ilifanikiwa kutekeleza miradi mbali mbali katika idara na taasisi zake, ikiwemo uimarishaji wa maeneo ya Kihistoria ya Mvuleni, Mwinyimkuu na Mkame Ndume, awamu ya pili iliotengewa shilingi 300,000,000/’.
Alisema katika eneo la kihistoria la Mvuleni, mjenzi kampuni ya KIN INVESTIMENT tayari amesafisha eneo lote la mradi pamoja na kujenga jingo jipya la kutolea huduma pamoja na vyoo vitakavyotumiwa na wageni watakaofika eneo hilo.
Aidha, alisema katika kipindi hicho Wizara ilipokea ujio wa ndege kadhaa, ikiwemo kutoka nchi za Russia, Uganda na Poland ambazo zimekuwa zikifanya safari za moja kwa moja kutoka nchini mwao hadi Zanzibar.
Vile vile alisema Wizara kupitia Wakala wa Uchapaji wa serikali imeanza kujenga jengo la ghorofa mbili linalotarajiwa kuwekwa mitambo mipya na ya kisasa, ukiwemo mtambo wa kuchapisha madaftari ya wanafunzi wa Serikali.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment