BENKI ya Watu wa Zanzibar (PBZ), imeanzisha akaunti maalum na kutoa mikopo ambayo itawawezesha waumini wa dini ya kiislam nchini kwenda kutekeleza ibada ya hijja inayofanyika mwaka mara moja huko nchini Saudi Arabia.

Kauli hiyo imetolewa na ofisa masoko wa benki hiyo Mohamed Khamis Ismail huko katika maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa (saba saba) yanayoendelea katika viwanja wa Mwalimu Nnyerere jijini Dar es Salaam ambayo yamezishirikisha nchi zaidi ya 30 duniani.

Alifahamisha kuwa benki hiyo imeanzisha akaunti maalum inayojulikana kwa jina la ‘hajj account’, ambayo itawawezesha waumini wa dini ya kiislamu wenye nia ya kwenda kutekeleza ibada ya hijja nchini Saudi Arabia.

Ofisa huyo alisema kwamba kupitia akaunti hiyo, muumini ataweza kuweka kidogo kidogo hadi pale zitakapofikia kiwango kinachotakiwa na kwenda kutekeleza ibada hiyo na hata anaweza kukopeshwa ili aweze kutekeleza ibada hiyo.

Akizungumzia mikopo kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada ya hijja (Hajj financing), Mohammed alisema vigezo vya kupata mkopo huo ni kuwa mteja wa benki hiyo na kujua vyanzo vya mapato ya mkopaji ili kuweza kuhakikisha mkopo unarejeshwa kwa wakati.

“Mfano kuna mtu anasubiri mafao yake ya pensheni na ana nia ya kwenda kufanya hijja na pensheni yake imechelewa pia tunamsaidia na pindi atakapo rudi atarejesha kiwango cha mkopo aliochukua”, alisema.
chanzo,Zanzibarleo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top