RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza kampuni ya mawasiliano ya ZTE ya China kwa kuunga mkono azma ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza mradi wa serikali mtandao (e-Government), ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia na kuimarisha utendaji serikalini.

Dk. Shein aliyasema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa kampuni ya mawasiliano ya ZTE kutoka nchini China ukiongozwa na makamu mkuu wa rais wa kampuni hiyo Zhao Peng.

Alimueleza kiongozi huyo na ujumbe wake kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhishwa na hatua za utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa serikali mtandao (e-Goverment) na kueleza mipango inayoendelea katika kuanza awamu ya pili.

Alisema mchakato wa kuanza kwa awamu ya pili ya mradi unaendelea kukamilishwa ambapo utahusisha uanzishwaji wa mfumo wa huduma za afya kwa njia ya kielektroniki (e-Health) na uanzishwaji wa mfumo wa kodi (e-Tax).

Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za umma na kuimarisha matumizi ya (TEHAMA), hali ambayo itaifanya Zanzibar nayo kuingia katika mabadiliko ya kiteknolojia.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo umuhimu wa   mfumo maalum kwa watendaji kutoka katika sekta hizo husika ili irahisishe utendaji wa shughuli hizo zitakapoanza.

Alieleza kuwa kwa vile teknolojia hiyo ni mpya na muhimu hapa nchini, hivyo suala la kupatiwa mafunzo kwa watendaji husika linapaswa kupewa kipaumbele huku akiipongeza kampuni hiyo kwa mafanikio iliyoyapata.

Nae makamu mkuu wa  rais wa kampuni ya kimataifa ya mawasiliano ya ZTE kutoka nchini China, Zhao Peng alimpongeza Dk. Shein kwa ushirikiano mzuri uliopata katika kutekeleza majukumu yake kwenye awamu ya kwanza ya mradi.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top