WANAWAKE wana mchango mkubwa katika kutekeleza majukumu ili kuziimarisha familia zao.

Akizungumza katika maadhimisho ya ‘Siku ya Wanawake Duniani’ yaliyofanyika jana Machi 8, 2018 katika kijiji cha Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, amesema wanawake ni nguzo muhimu ya kuinua familia.

Amesema akinamama wana mchango mkubwa katika kuimarisha familia ili zipate ustawi na kuzifanya zipige hatua zaidi ya maendeleo nchini.

Hata hivyo, ameeleza kuwa wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa kila kunapotokea matatizo nchini yenye mwelekeo wa kupoteza amani.

Kwa hivyo amesisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano katika kuendeleza amani na mshikamano ili kuhakikisha wanawake na watoto wanakuwa salama na kuishi bila khofu.

Aidha, Mama Shein aliwataka akinamama na akinababa kushirikiana katika malezi bora ya watoto kulingana na maadili, silka na utamaduni wa nchi ili wawe raia wema.

Kuhusu vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyoendelea kushamiri kwa kasi, Mama Mwanamwema alisema Zanzibar bila ya uovu huo unaoathiri maendeleo ya taifa inawezekana iwapo jamii itakuwa kitu kimoja kwa kushirikiana kuvikomesha 

Sambamba na hayo, alisema katika kupinga mapambano dhidi ya maradhi ya ukimwi, wanawake wana mchango mkubwa wa kudhibiti maambukizo ya virusi ifikapo mwaka 2030.

Lakini alieleza kusikitishwa kwake na kiwango kikubwa cha wanawake wanaoambukizwa maradhi hayo ambako kiko juu kuliko kwa wanaume.

“Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini ni mara mbili ya wanaume, hivyo tuchukuwe hatua madhubuti za kujiepusha na vitendo vinavyochangia kupata maradhi hayo,” alisisitiza.

Aidha aliwataka wanawake kuzitumia fursa za kujiunga na vikundi vya ushirika ili kujiimarisha kiuchumi kwa kujiongezea kipato na kupambana na umasikini, hali itakayoipa nguvu Serikali na washirika wengine kutanua wigo wa misaada yao. 

Kwa upande wake, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Mhe. Maudline Cyrus Castico, alisema wakati umefika kwa wanawake kushirikiana katika kuleta mabadiliko vijijini ili kufikia ukombozi wa kiuchumi.

Alieleza kuwa, wanawake wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo nchini, hatua inayoweza kuwafanya wajielewe na kujitambua.

Castico alikemea tabia iliyoanza kujitokeza sasa ambapo baadhi ya watu na makundi huwakamata wanawake na watoto, kuwapiga na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kuwabaka.

Siku ya Wanawake kimataifa, iliasisiwa na Umoja wa Mataifa kupitia mkutano uliofanyika mwaka 1995 jijini Beijing China, ambapo ujumbe wa mwaka huu ni, “Wakati umefika tushirikiane kuleta mabadiliko ya wanawake vijijini”.
Mwisho

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top