WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye mashindano ya klabu bingwa na kombe la shirikisho Afrika,timu za JKU na Zimamoto, juzi zimetolewa katika mashindano hayo baada ya kufungwa kwenye michezo yao ya ugenini.

JKU iliyosafiri hadi katika jiji la Ndola Zambia kucheza na mabingwa wa huko ZESCO, ilichapwa kwa aibu mabao 7-0 katika mchezo wa upande mmoja uliochezwa kwenye uwanja wa Mwanawasa.

JKU inakuwa timu ya pili kutoka Zanzibar kufungwa mabao mengi katika mashindano hayo, baada ya polisi ambayo ilikuwa kuiwakilisha Zanzibar katika michuano hiyo, kufungwa mabao 6-0 na Etoile Du Sahel ya Tunisia mwaka 2006 na kubatizwa jina la ‘Wazee wa Tunisia’.

Katika mchezo huo, JKU iliyoonekana kucheza kwa kutojiamini ilizidiwa katika maeneo yote na kuwapa nafasi wenyeji kufanya mashambulizi ya mara kwa mara.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa uwanja wa Amaan Februari 10, JKU ililazimishwa sare ya 0-0.

Nchini Ethiopia, Zimamoto ilifungwa bao 1-0 na wenyeji Wolaita Dicha katika mchezo wa kombe la shirikisho uliochezwa mjini Hawassa na kutolewa kwa tofauti ya mabao 2-1 baada ya mechi ya kwanza iliyochezwa uwanja wa Amaan Februari 11 kutoka sare ya 1-1.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top