Mamlaka ya Udhibiti wa  huduma za Maji, nishati na Mafuta Zanzibar  ZURA  imesema upungufu wa mafuta ya Petroli uliojitokeza nchini katika vituo mbalimbali Zanzibar  unatokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma hiyo  kwa wananchi.

Akizungumza na Zanzibar24 huko Ofisini kwake Maisara mjini unguja,  Afisa Habari wa Mamlaka hiyo Mbaraka Hassan Haji amesema  kiwango cha mafuta  kilichotengwa kutumika kimekuwa kidogo  ukilinganisha na mahitaji ya wananchi hasa  katika kipindi hichi cha skukuu ya mwaka mpya.

Amesema kampuni za mafuta  ikiwemo United Petrolium, Gapco huwaagiza mafuta kulingana na kiwango  cha matumizi wanachokihitaji katika bohari zao za kuhifadhia mafuta lakini kiwango hicho  kilizidiwa  kutokana na mahitaji kuongezeka zaidi kwa wananchi.

Aidha amesema kwa mwaka huu mpya 2018  Mamlaka imeweka mikakati kuhakikisha   tatizo la  uhaba wa mafuta  linadhibitiwa  ili lisiweze kujitokeza  ambapo  wameahidi kukaa chini na makampuni ya mafuta yanayotoa  huduma za mafuta  visiwani Zanzibar ili kushirikiana.

Hata hivyo amesema bado mamlaka inakabiliwa na tatizo la  sehemu ya kuhifadhia mafuta  kulingana na mahitaji lakini serikali imeshafanya  hatua za kutafuta eneo ambalo litatumika  kwa ajili ya kuhifadhia mafuta ili liweze kukidhi na kutoa huduma hiyo bila ya usumbufu wowote.

Chanzo, Zanzibar 24

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top