Watu zaidi ya 10 wakiwemo waliovaa sare za askari Magereza
wamevamia baa moja iliyopo Keko jijini Dar es salaam, kujeruhi watu huku
wakipora mali mbalimbali zikiwemo simu za mkononi na fedha za wateja.
Watu hao walivamia baa hiyo iitwayo Omax jana saa tano usiku na
kuanza kuwapiga na kuwapora mali hizo wateja kisha kutokomea gizani.
Awali, kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema
alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi, alisema yuko Kibiti
kikazi. Hata hivyo alikiri kupigiwa simu usiku wa siku ya tukio na watu
wakitaka kupatiwa fomu za PF3 kwa ajili ya matibabu.
“Nilipigiwa simu na watu wengi wakitaka kupatiwa PF3 wameumia,
nikawaambia niko mbali waende tu Kituo cha Polisi Chang’ombe
watasaidiwa, sasa sijui walienda ama vipi na sasa hivi siwezi kutoa
ufafanuzi kwa sababu niko Kibiti kikazi,” alisema.
Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Agustine Mboje
alisema taarifa ya kuvamiwa kwa baa na watu kupigwa hana, lakini
anachofahamu kuna askari wao alivamiwa na vibaka na kupigwa wakati
akienda kazini, kisha wakatoa taarifa Kituo cha Polisi Chang’ombe.
Mboje alisema baada kutoa taarifa, polisi wakishirikiana na askari
Magereza walifanya msako kuwatafuta na kuwakamata baadhi ya vibaka ambao
waliwafikisha katika kituo hicho.
Mhudumu wa baa iliyovamiwa aliyejitambulisha kwa jina moja la Mary
alisema walifika watu zaidi ya 10 wakiwa wameshika mikanda wakaanza
kuwapiga watu, lakini alipoona hivyo alikimbilia chooni akiwa na mteja
ambako walifuatwa na kuanza kupigwa.
Alieli Nelson aliyekuwa mteja ambaye alijeruhiwa kichwani, alisema
walikuwa kwenye baa hiyo wakisubiri chakula na ghafla walivamiwa na
kundi la watu wakiwa wamevalia sare za askari Magereza na wengine wakiwa
wamevaa kiraia.
Chanzo, Zanaibar 24
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment