MCHANA wa jana ulikuwa ni zamu ya  Timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka la Ufukweni ‘Zanzibar Sand Heroes” kualikwa chakula cha mchana pamoja na kupewa zawadi ya kuanzia ya TZS milioni moja kwa kila mchezaji pamoja na viongozi wa timu hiyo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk. Shein aliwaahidi wachezaji na viongozi wa Timu hiyo ambao ni mabingwa mwaka huu wa mchezo huo kuwa zawadi nyengine ya aina yake atawakabidhi baada ya kushauriana na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akiwaalika katika Taarab rasmi ya Kikundi cha Taifa itakayofanyika usiku wa Januari 12, mwaka huu ikiwa ni madhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Hafla hiyo ya chakula cha mchana ambayo Dk. Shein amewaandalia wachezaji na viongozi wa timu hiyo, ilifanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali vyama vya siasa na michezo pamoja na Serikali na wanamichezo wengine wakiwemo veterani.
Katika hotuba yake fupi mara baada ya chakula hicho cha mchana, Rais Dk. Shein alisema kuwa  ni muhimu kukutana na timu hiyo  kutokana na kazi nzuri waliyoifanya baada ya kwenda katika mashindano hayo na bendera ya Zanzibar na kuiwakilisha vyema katika mashindano hayo na hatimae kuwa washindi kwa kuishida Malawi jumla ya mabao 3-2.
Alieleza kuwa timu hiyo imefika hatua kubwa na kueleza furaha yake kwa timu hiyo kwa manafanikio makubwa kwa nafasi ya 20 na pointi tatu katika nchi za Afrika huku akieleza kuwa na tayari Zanzibar imeshasajiliwa rasmi na chama cha mpira cha Afrika kinachoendesha mashindano hayo.
Pia, alieleza kufarajika kwa  nafasi ya Zanzibar katika FIFA  pamoja na kusajiliwa rasmi na FIFA huku ikiwa inatambulikana Kitaifa na Kimataifa na kueleza kuwa wasije kushangaa kuona timu ya  Brazili inakuja hapa nchini kucheza na timu ya Taifa ya Zanzibar kutokana na nafasi iliyonayo Zanzibar hivi sasa katika mashindano hayo.
“Kwa vile maandalizi yalikuwa haraka haraka nimeamua kukupeni zawadi hii ndogo na baadae nitakupeni zawadi nyengine na kwa kawadia yangu mimi ninakuwa sisahau... na zawadi ya pili naitia mfukoni  nataka kushauriana na viongozi wa serikali halafu nitakupeni” alisema Dk. Shein ambaye yeye mwenyewe aliwahi kuwa mwanamichezo mahiri hapa Zanzibar.
Alisema kuwa Wazanzibari wakiwemo viongozi wamefarajika sana na ushindi wa timu hiyo na kueleza kuwa kwa kawaida wachezaji wazuri wa mpira wanatokana katika timu hizo kwani wachezaji wengi maarufu duniani wametoka katika timu za mpira za ufukweni na kueleza matumaini yake kutokea wachezaji kutoka kwenye timu hiyo watakaoingia kwenye timu ya “Zanzibar Heroes”.
Dk. Shein, alieleza matumaini yake kuwa Zanzibar itaimarika zaidi katika timu ya taifa ya mpira wa miguu pamoja na timu ya taifa ya ufukweni.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa mwezi wa Februari timu kutoka Afrika Kusini inatarajiwa kuja kucheza na timu hiyo katika mashindano ya kirafiki hatua ambayo inaimarisha na kuendeleza utalii kama ilivyo kwa nchi zenye fukwe duniani ambazo nyingi zimo katika mashidano hayo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alipokea ombi la kuwa mlezi wa timu hiyo na kueleza kuwa atahakikisha maandalizi ya hapo mwakani yanakuwa mazuri zaidi.
Alieleza kuwa timu hiyo kama ilivyo kwa “Zanzibar Heroes” kuna haja ya kuzilea na kuzisaidia kwani ni timu za Zanzibar na wachezaji wake wamekuwa wakifanya vizuri na hasa katika vilabu vyao vya nje kutokana na uwezo wao. “Zile nguvu waliozaniwa wamezipata katika mambo mengine wanazizihirisha ”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa Serikali itakuwa pamoja na timu hiyo na itaandaa programu kutokana  na ushauri wa Kocha Adof na kuahidi kuwa atahakikisha wanakwenda kwenye mashindano wakiwa kifua mbele.
Aliwataka wachezaji hao kuwa kitu kimoja, kuwa marafiki na kuwa imara na waweze kusaidiana kwani michezo kwa kawaida hujenga udugu na urafiki mkubwa kama alivyo yeye na wanamichezo aliocheza nao ukiwemo mpira wa miguu na riadha ambao wako pamoja hadi hivi leo
Mapema akisoma risala ya Timu hiyo ya Taifa ya “Zanzibar Sand Heroes”, kocha mkuu wa timu hiyo Ali Sharif Adof alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, BTMZ, ZFA na Kamisheni ya Utalii kwa kuweza kuwaunga mkono hadi kuweza kushiriki mashindano na kurudi na ushindi katika mashindano hayo yaliyofanyika huko Tanzania Bara kuanzia tarehe 24 hadi 26 Disemba mwaka jana.
Alieleza kuwa katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu nchi mbali mbali zilishiriki ikiwemo Malawi, Uganda na wenyeji wa mashidnano hayo Tanzania Bara pamoja na timu yao kutoka Zanzibar.
Uongozi wa timu hiyo ulieleza kuwa kama anavyosisitiza Rais Dk. Shein  kuwa hadhi ya michezo anataka irudi kama zamani basi vijana wake hao wapo tayari kwa hali na mali kuirejesha hadhi hiyo ya michezo hapa Zanzibar.
Adof alieleza kuwa kama walivyoonesha ndugu zao wa “Zanzibar Heroes”  na wao wakapata ari ya kucheza kwa nguvu zote hivyo, walitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa dhati wanamichezo wenzao hao kwa ushindi wao walioupata kwani wamejitolea kwa moyo wao uzalendo kuhakikisha kwamba wanailetea usndi Zanzbar.
Pamoja na hayo alieleza kuwa Zanzibar katika mchezo huo inatambulikana FIFA na CAF kama nchi ambapo kabla ya mashindano hayo kwa upande wa kimataifa Zanzibar iko nafasi ya 100 kati ya nchi 113 ambapo kwa Afrika iko nafasi ya 20 katika ya nchi 56.
“Tunakupongeza Mheshimiwa Rais kwa namna unavyoshughulikia maendeleo ya sekta ya Utalii nchini pia kwa juhudi zako za kuirudisha tena hadi ya Zanzibar katika michezo hatua cha kukupa ili tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu afya njema maisha marefu na mafanikio ya hali ya juu katika utekelezaji wa kazi za Urais” ilisema risala hiyo iliyosomwa na Kocha mkuu Adof.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top