RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeimarisha mfumo wa takwimu kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo.

Dk. Shein aliyasema hayo jana baada ya kuzindua jengo jipya la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, liliopo Mazizini  ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Alisema serikali zote mbili zinahitaji takwimu ili ziweze kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa uhakika kwani ndizo zinazowesha kujipima na kujitathmini na kufanya maamuzi sahihi.

Alieleza kuwa takwimu zilizokusanywa vizuri ni msingi muhimu katika kuimarisha utoaji wa huduma bora na kuendeleza misingi ya utawala bora.

Aliongeza kuwa ukusanyaji wa takwimu sahihi na kwa wakati mzuri ni changamoto katika nchi nyingi duniani na  kutumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kujiimarisha zaidi hivi sasa na kuweza kutoa takwimu kwa wakati.

Aidha aliitaka ofisi hiyo kuongeza kasi katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusiana na takwimu na umuhimu wake kwa jamii na kuipongeza Ofisi hiyo kwa juhudi zake.

Dk. Shein aliigiza wizara ya Fedha na Mipango kuongeza kasi katika kuwasomesha wafanyakazi ili kuwepo wataalamu wa kutosha wa masuala ya takwimu.

Alisisitiza haja ya mambo ya Muungano kuendelea kufanywa kwa mashirikiano ya pamoja kwa pande zote mbili ili kuweza kupata mafanikio makubwa zaidi.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa kutekeleza agizo lake la kuandaa Semina ya Takwimu ambapo agizo hilo lilitekelezwa kwa kipindi kifupi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa juhudi za kujenga majengo ya kisasa zinakwenda sambamba na utekelezaji wa Mipango Miji iliyokwishaanzwa huku akizihimiza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga miji ya kisasa katika maeneo ya Kwahani, Mkokotoni, Chumbuni na Chwaka.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo nafuu wa fedha na ushauri muhimu ulioweza kufanikisha ujenzi huo na kuwashukuru wahisani wakiwemo Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Serikali ya Canada, GAC na EU kwa michango yao waliotoa katika utekelezaji wa Mkakati Kabambe wa Kuimarisha Takwimu Tanzania.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohamed alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuhakikisha suala zima la takwimu linapewa kipaumbele huku akieleza mafanikio ya takwimu hivi sasa sambamba na hatua za kuvuka lengo la kuingiza watalii 500,000 hapa Zanzibar.

Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Ashatu Kijaji alimpongeza Dk. Shein na kueleza kuwa mwaka 2006 akiwa Mamaku wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua utayarishaji wa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuimarisha Takwimu nchini (TSMP) na hatiae mwaka 2010 Serikali iliridhia kwa kipindi cha miaka mitano.

Mapema Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika hotuba yake alieleza kuwa jengo hilo lenye ghorofa nne limejengwa na kusimamiwa na Kampuni za kizalendo kutoka Tanzania ambapo Kampuni ya ujenzi  ya Worid Class Engeneering and Construction Limited yenye makao makuu yake Tanzania Bara na Kampuni ya Y&Architects Ltd ilisimamia shughuli za ujenzi huo.

Alieleza kuwa Ujenzi ulianza mwezi Februari 2016 na kukabidhiwa rasmi kwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, 2017 ambao umegahrimu jumla ya TZS Bilioni 7.9.

Aliongeza kuwa jengo hilo lenye vymba 60 litakidhi mahitaji ya watumishi wapatao 150 na hivyo kuondoa kabisa changamoto iliyokuwepo ya uhaba wa nafasi na mazingira bora ya sehemu za kufanyia kazi.

Nae Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia Bi Bella Bird alieleza haja kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwaandalia mafunzo wafanyakazi wa takwimu ili waweze kufanya kazi zao kwa ustadi zaidi.

chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top