BAADHI ya wanaharakati wa kupinga masuala ya udhalilishaji Mkoa wa Kaskazini Unguja wamesema suala la kutiwa hatiani washitakiwa wa makosa ya udhalilishaji na kufungwa kwa muda baadae wakaonekana mitaani ni jambo linalowavunja moyo.

Sambamba na hilo walisema kuwa watu wengi ambao wamehukumiwa vifungo hukaa gerezani takribani wiki mbili ama tatu na kutolewa bila ya taarifa kwa wahanga wa matukio hayo.

Walisema kuwa kuweko kwa hali hiyo kunawakatisha tamaa wananchi na hivyo kuwapa mwanya watendaji wa makosa hayo kuendelea.

Akizungumza na gazeti hili huko Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa niaba ya wanaharakati wenziwe, Hadia Ali Makame, alisema kuna kesi nyingi za kubakwa ndani ya mkoa huo ambapo watendaji wa makosa hayo wametiwa hatiyani lakini cha kushangaza wametumikia adhabu kwa muda mfupi.

“Kuna kesi zaidi ya nane nnazozikumbuka kwa haraka ambazo wafanyaji wake baadhi yao walifungwa miaka saba wengine mitano lakini wote hao hata mwaka mmoja hawakufika ndani wametoka na nyengine tumekwenda kukata rufaa, lakini tulikwenda na kurudi mwisho tumechoka hakuna mafanikio,”alisema.

Mwanaharakati huyo ambae ni Katibu wa Jumuiya ya JUWAMAKU, alisema hali hiyo inakatisha tamaa kwao pamoja na wananchi kwani hutumia muda na gharama kufatilia kesi hizo mwisho wake wafanyaji wanadunda mitaani.

Nae Nyange Vuai Haji ambae mjukuu wake alibakwa alisema mjukuu wake akiwa na umri wa miaka 11 alibakwa na kesi ilifikishwa sehemu husika na mshitakiwa alifungwa miaka saba lakini matokeo yake alikaa ndani kama wiki mbili na kuachiwa.

Alisema yeye aliumia kuona hali hiyo, lakini hakuwa na lakufanya kwani yeye hakuwa na uwenyeji wa kuweza kufuatilia tena kesi hiyo,chanzo Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top