WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud, amesema vyama vingi sio chuki wala kupandikiza fitina ndani na nje ya nchi, bali ni jambo la kushindana kwa hoja zitakazochangia maendeleo ili kutimiza azma ya mapinduzi ya mwaka 1964.

Alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wananchi pamoja na baadhi ya watendaji wa serikali huko Mkokotoni mkoa wa Kaskazini Unguja katika muendelezo wa shamrashamra za Mapinduzi.

Alisema sio vizuri kwa viongozi kuwa na tabia za kusambaza chuki, ubaguzi pamoja na kuwagawa watu kwa utashi, tamaa na ubinafsi badala yake ni kujenga hoja zenye kuleta tija kwa wananchi na taifa kwa jumla.

Aidha alisema ni busara kwa baadhi ya viongozi kutambua kwamba hakuna taifa wala taasisi yoyote yenye uwezo wa kuubadilisha uongozi wa Zanzibar kwa maneno, hivyo ni vyema kuungana na serikali katika uimarishaji wa maendeleo.

Aboud alisema, kiongozi bora ni yule mkweli, muadilifu na mwenye kuchapakazi kwa ajili ya maendeleo na hiyo ndio dira sahihi ya mapinduzi ya mwaka 1964.

“Wanayoyakebehi na kuyakejeli mapinduzi hayo wameishia na kuhangaika na dunia tu huku wakiendelea kupoteza heshima na thamani yao kwa wazanzibari waliowengi na hata wale waliokuwa wakiwaamini”,alisema.

Aliongeza,“ukiyapokea mapinduzi yatakupokea na kuyakataa nayo yatakukataa wapo baadhi ya viongozi waliyoyakataa mapinduzi wamekuwa wakihangaika na ulimwengu”.

Kuhusu maendeleo alisema, serikali zote zimekuwa zikisimamia malengo na azma ya muasisi wa mapinduzi marehemu Abeid Amani Karume katika kuwaletea maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi wananchi wake.

Alisema hatua hiyo inapaswa kuenziwa na kuendelezwa kwani ndio sera ya Afro-Shirazi Party na kwa misingi hiyo ni vigumu kukiondoa madarakani chama cha mapinduzi kimepata baraka za Afro-Shirazi,chanzo Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top