MAKOSA 219 ya udhalilishaji yameripotiwa katika mkoa wa Kaskazini Unguja kwa mwaka 2017.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mahonda Kamanda wa Polisi Mkoa huo Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hasina Ramadhan Taufiq, alisema kati ya makosa hayo kesi tano zilipatikana na hatia mahakamani na wafanyaji wa vitendo hivyo wamehukumiwa vifungo.

Alisema, kati ya kesi hizo saba zilifutwa kutokana na kukosekana ushahidi na makosa 18 zimefungwa polisi kutokana na kukosekana ushahidi wa kutosha, kesi 13 zinaendelea mahakamani huku majalada manne yanasubiri majibu ya kipimo cha DNA kwa waathirika walipatiwa ujauzito.

Aidha, alisema katika kesi hizo nyingi upande wa mtuhumiwa na muathiriwa kumalizana kifamilia hali ambayo inarejesha nyuma jitihada za serikali za kupambana na matendo hayo.

Kamanda Hasina, alisema kesi 139 zinaendelea na upelelezi huku majalada 33 yapo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.

Akiwataja waliohukumiwa katika kesi hizo ni Haji Zidi Haji ambae alipata kifungo cha miaka mitatu jela, Hemed Mahmoud Said miaka mitatu, Abdul-rahman Haji Bakari mkaazi wa Mkwajuni kufungwa siku 90, Khamis Makame Foum miaka mitatu wote wakitiwa hatiani kwa kosa la kutorosha na Salum Mohammed Salum kuhukumiwa kifungo cha miaka saba kwa kosa la kutorosha na kumuingilia msichana kinyume na maumbile.

Alisema mkakati wa jeshi la polisi katika kesi za udhalilishaji kwa mwaka huu kuhakikisha zinapelelezwa ipasavyo na hakuna jalada litakalofungwa ndani ya polisi kwani makosa hayo yanaweza kusababisha madhara mbalimbali kwa mtu aliefanyiwa vitendo hivyo.

Mkakati mwengine ni kutoa elimu kwa masheha ili kuona makosa hayo yanafikishwa polisi na badala yake hayamalizi katika ngazi za familia.

Hivyo aliziomba tasisi nyengine za serikali na zisizo za kiserikali kushirikiana pamoja ili kuona makosa hayo yanaondoka.

Akizungumzia makosa ya dawa za kulevya alisema jumla ya kesi 95 zimeripotiwa ambapo kesi 47 zilihusisha watu kukamatwa na dawa za kulevya na kesi 48 zilihusisha watu kupatikana na bangi.
Chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top