CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar  kimesema mafanikio yliyofikiwa na Serikali ya awamu ya Saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein ni kielelezo tosha cha kuenzi kwa vitendo  Mapinduzi hayo ya Januari 12, mwaka 1964.

Udhibitisho huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ wakati akitoa tathimini yake juu ya hotuba ya Rais wa Zanzibar Dk.Shein aliyoitoa katika kilele cha  wamaadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi   zilizofanyika Uwanja wa Amaan Mjini hapa.

Dk. Mabodi alisema mambo yaliyotajwa katika hotuba hiyo ni sehemu ya mafanikio ambayo kila mwananchi anatakiwa kujivunia kwani ni hatua ya maendeleo yanayotokana na utekelezaji  mzuri  wa Ilani ya Uchaguzi  CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote.

Alisema serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar imetekeleza mambo mbali mbali ya kimaendeleo bila kujali changamoto na vikwazo vya kisiasa kwa lengo la kurahisisha upatanaji wa huduma za msingi kwa wananchi waliopo mijini na vijijini.

Alieleza kuwa mambo yaliyotolewa ufafanuzi wa kina ndani ya hotuba hiyo ya Dk.Shein ni pamoja na kuimarika kwa sekta ya uchumi ambapo makusanyo ya mapato yamefikia shilingi bilioni 548.571 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na shilingi bilioni 487.474 zilizokusanywa katika mwaka 2016.

Alisema kwa mujibu wa hotuba hiyo imetaja kasi ya ukuaji wa uchumi kwa bei halisi imekua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2017, ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016, hatua inayopongezwa na Chama cha Mapinduzi Zanzibar.

Naibu Katibu mkuu huo anaendelea kueleza kuwa kutokana na juhudi za serikali chini ya usimamizi wa CCM pato la mtu mmoja limetajwa kufikia shilingi 1,806,000 ikilinganishwa na shilingi 1,632,000 kwa mwaka 2015.

Pia alieleza kuwa kasi ya mfumuko wa bei imefikia asilimia 5.6 katika mwaka 2017 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2016.

“Mafanikio yote hayo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi tulizotoa kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar  wakati wa Uchaguzi Mkuu wa dola uliopita kwa hiyo tunaendelea kutekeleza  kwa kasi kubwa ili ikifikia uchaguzi mkuu ujao tuwe tupo katika kiwango cha kuridhisha katika utatuzi wa kero za wananchi.”, alisema Dk.Mabodi.

Alisema  lengo la serikali ni kuhakikisha ni kuimarisha uchumi,kupunguza umasikini na kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kiwango cha kati ifikapo mwaka 2020 huku ikijipanga kufikia kiwango cha nchi za visiwa zilizoendelea duniani.

Dk.Mabodi aliisifia serikali kwa hatua zake za miradi mikubwa 25 ambayo ikikamilika itatoa ajira 915 kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar.

Akizungumzia sekta mama ya Utalii nchini alisema katika hotuba ya Dk.Shein imeweka wazi kuimarika kwa Nyanja hiyo ambayo imeingiza jumla ya watalii 433,116 nchini katika kipindi cha mwaka 2017,ikilinganishwa na idadi ya watalii 379,242 walioingia nchini katika mwaka 2016 ambalo ni ongezeko la asilimia 14.2.

“Sina shaka na ahadi ya Rais wetu mpendwa Dk.Shein ya Serikali kufikia idadi ya watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020”,, Dk.Mabodi alipongeza juhudi hizo na kutoa wito kwa wananchi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha dhana ya utalii kwa wote.

Pamoja na hayo Dk.Mabodi alisema serikali chini ya usimamizi wa CCM  imekuwa mstari wa mbele kuimarisha sekta ya Elimu ambayo ni chimbuko na uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yoyote duniani kwa kuzalisha wataalam wa fani mbali mbali wanaosaidia kutekeleza sera za kisiasa ili ziendane na mahitaji halisi ya wananchi.

Kupitia tathimini ya hotuba hiyo Dk.Mabodi alisifia tamko la Rais wa Zanzibar  Dk.Ali Mohamed Shein la kuwatangazia wananchi kuwa kuanzia mwezi wa Julai 2018, serikali itaanza kutekeleza azma ya kurudisha utaratibu wa elimu bure kwa ngazi za msingi na sekondari  ili kutekeleza shabaha ya Mapinduzi.

Mbali na tamko hilo pia Dk.Mabodi alisema CCM inaunga mkono msimamo wa Serikali kutoa pencheni jamii kwa wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 , bila kuzingatia kazi walizokuwa wakifanya  ambapo jumla ya wazee 27,627 wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 10.175 tangu utaratibu huo umeasisiwa mwezi  April 2016, kwa kila Mzee kupewa  sh.20,000 kwa mwezi.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi alifafanua kuwa suala la maendeleo halitakiwi kuchanganywa na tofauti za kisiasa, kidini na kikabila kwani linawahusu wananchi wote hivyo wasikubali baadhi ya wanasiasa waliofilisika kwa hoja wawagawe kupitia kivuli cha siasa zilizopitwa na wakati.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top