UMOJA wa Walimu Wakuu wa skuli zenye kidato cha sita Zanzibar, unakusudia kuongeza ufaulu wa madaraja ya juu kwa watahiniwa wa mitihani ya taifa ya kidato cha sita.

Mkuu wa taaluma wa skuli ya Benbella, Victor Tadel Clement, alisema hayo katika skuli ya Mpendae kwenye  mkutano wa kujadili na kubadilishana mawazo ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani yao.

Alisema msukumo huo umekuja ni baada ya baadhi ya skuli kupata matokeo mabaya katika miaka iliyopita  ambapo  mwaka 2016 kati ya skuli 10 za mwisho kitaifa nane zilikuwa za Zanzibar na kwa mwaka 2017 katika skuli 10 za mwisho, saba zilikuwa ni za Zanzibar.

Alisema umoja huo utahakikisha unasimamia maendeleo ya wanafunzi wao pamoja na kujadili kwa pamoja changamoto zinazozikabili skuli zao.

Alisema lengo la umoja huo ni kuhakikisha ufaulu unaongezeka zaidi na kuondoa idadi kubwa ya watahiniwa wanaopata daraja la nne na sifuri.

Mwenyekiti wa umoja huo, Mussa Abdi Khamis, alisema katika kuondoa changamoto hiyo, umoja huo utahakikisha wanafunzi wanafaulu kwa madaraja ya kwanza, pili na tatu.

Alisema jambo jengine ni kuhakikisha kila mwalimu anamaliza mtaala aliopangiwa kabla ya mitihani na wanafunzi kuandaliwa vyema kukabili mitihani yao.

Pia alisema walimu wote watakaguliwa na wakaguzi wa elimu sambamba na kufanya mitihani ya pamoja kwa skuli zote zenye kidato cha tano na sita.

chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top