SERIKALI imesema haijafikiria kuacha kusherehekea mapinduzi ya mwaka 1964 kwani ndiyo yaliyomkomboa mwananchi mnyonge kutoka kwenye minyororo ya ukoloni.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisi kwake Vuga.

Alisema sherehe za mapinduzi zinajenga dhamira njema ya maendeleo na msingi wake tokea awali ni kuleta maendeleo ya haraka zaidi nchini.

“Tukisema leo tuache historia yetu hii maana yake ni sehemu ya kurejesha nyuma maendeleo yetu na kupoteza fikra, busara na hekma za marehemu mzee Karume ambapo msingi wake mkuu wa kufanya mapinduzi ni kuwakomboa Wazanzibari waonynge,”alisema.

Alisema jambo hilo ni la kihistoria na hakuna nchi yoyote duniani inayosahau siku yake ya kitaifa.
“Hatuwezi kuacha kujikumbusha namna ya kufanikisha maendeleo yetu ambayo ni sehemu ya kipimo cha kila mwaka, kabla ya mapinduzi visiwa vyetu vilikuwa katika hali mbaya,” alisema.

Mbali na hayo alisema serikali inaposherehekea sherehe hizo si kama inatumia pesa kinyume na utaratibu bali inatumia kwa ajili ya kujenga misingi imara ya kuendeleza maendeleo kwa wananchi.
“Haya yote tunayoyafanya ni kwa ajili ya kufunza vizazi vipya vielewe mapinduzi yeyewe, muelekeo wetu na kuona taifa letu linazidi kupiga hatua kwa msingi wa maendeleo kijamii, na kisiasa,” alisema.

Hivyo, aliwasisitiza wananchi kutembea kifua mbele katika kuyaendeleza mapinduzi yao kwa mafanikio ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia mapambano dhidi ya udhalilishaji, alisema katika kuelekea miaka 54 ya mapinduzi serikali imejipanga kukabiliana na tatizo hilo kwa  kuhakikisha linaondoka.

Alisema hatua na mipango mbalimbali inachukuliwa ambapo kwa kiasi kikubwa imeweza kusaidia kupunguza tatizo hilo  ikiwemo wananchi kujitokeza kuripoti matukio ya udhalilishaji.

chanzo, Zanzibae leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top