WATENDAJI na watumishi wa hospitali kote nchini, wametakiwa kuacha tabia ya kuuza damu kwa wenye mahitaji, kwa sababu kitendo hicho kinakwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa benki ya damu.

Waziri wa Afya, Hamd Rashid Mohammed, alisema hayo wakati akifungua juma la mamlaka ya mafunzo ya amali, katika viwanja vya mnara wa kumbukumbu ya mapinduzi Kisonge, ambapo pamoja na mambo mengine kulifanyika zoezi la kuchangia damu kwa hiari.

Juma hilo lilihusisha vikundi mbali mbali vya ujasiriamali, wanafunzi wa vyuo na wadau wa mafunzo ya amali.

Alisema kuna umuhimu wa mamlaka za afya kusimamia upatikanaji wa damu na kuhakikisha inatolewa bila malipo kwa wanaohitaji ili kuokoa maisha yao.

Aidha alizitaka hospitali na vituo vya afya kufahamu mahitaji halisi ya damu ili kuandaa mikakati ya kuikusanya.

“Cha msingi ni kujua tuna damu kiasi gani kwa matumizi ya leo na akiba, lakini pia tujiandae kuwa na damu ya kutosha kwa mwezi wa ramadhani kwa sababu mahitaji yanakuwa makubwa lakini inakuwa haipatikani,” alisema.

Aliitaka benki ya damu kupanua wigo wa kukusanya damu kwa kuwafikia wadau wengi zaidi, wakiwemo askari wa vikosi maalum, wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyakazi wa serikali na makundi mengine.

Akigusia mafunzo ya amali, alitaka kuwepo mfumo wa kujenga watu wenye uwezo kitaaluma katika kufanyakazi ili kuimarisha uchumi wa taifa.

Aliwaomba wananchi kuthamini kazi nzuri inayofanywa na serikali kwa kusaidia kujenga vituo vya amali kwa sababu kundi kubwa la vijana bado halijanufaika.

Katibu wa jumuiya ya uchangiaji damu Zanzibar, Makame Bakari Magarawa, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari, ili isaidie wagonjwa wanaopata matibabu hospitali hasa wanawake na watoto.

Zaidi ya chupa za damu 70 zilikusanywa katika hafla hiyo iliyovutia idadi kubwa ya wananchi.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top