SERIKALI imewasisitiza vijana kuzitumia fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwemo ajira, elimu, ujasiriamali na fursa za biashara ambazo zitawakwamua na hali ngumu ya maisha.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Rahma Ali Khamis, alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya elimu ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na mabara ya vijana ya Zanzibar yaliyofanyika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.

Alisema kama vijana watatumia fursa hizo basi watakuwa wanaunga mkono juhudi za serikali katika kujikwamua na umasikini na kusukuma mbele maendeleo ya nchi yao.

Aidha, alisema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ziko  mstari wa mbele kuwatafutia fursa za kiuchumi wananchi wake kupitia programu za jumuiya za kikanda.

Alifahamisha kuwa serikali inafahamu umuhimu wa kuwashirikisha vijana kama kiungo muhimu katika ngazi tofauti za jamii mijini na vijijini katika mambo ya maendeleo ikiwemo  elimu juu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema elimu hiyo ni pamoja na kuangalia namna bora zaidi ya kuwanufaisha wananchi pamoja na vijana kwa fursa za kibiashara na nyengine zinazopatikana katika jumuiya hiyo ili kuondoa umasikini na kunyanyua kipato chao.

Alibainisha kuwa kwa kuzingatia hali halisi kwa vijana ambao ndio mawakala wa kutunza utamaduni na bidhaa za kimagharibi hivyo ni lazima kuacha uwakala huo na kujenga tabia ya kupenda vya kwao kwani kufanya hivyo itasaidia kulinda viwanda.

Hata hivyo, alisema ifikapo mwaka 2024 Jumuiya ya Afrika Mashariki inatarajia kuanza utekelezaji hatua ya tatu ya mtanganao wa itifaki ya umoja wa safaru ambao nchi wanachama zitatumia sarafu moja ambayo itawezesha kufungua fursa nyingi za maendeleo kwa vijana na nchi wanachama.
chanzo, zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top