KUFUATIA juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima haitokei, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linamshikilia kiongozi mmoja kwa tuhuma za kuuza kiwanja cha serikali.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Madema, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Hassan Nassir Ali, alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Halima Salum Abdalla (51) mkaazi wa Fuoni Moroko.

Alisema, mtuhumiwa huyo alidaiwa kuwa akiwa na mwenzake alietambulika kwa jina Issa Mwinyi Khamis (32) mkaazi wa Fuoni walimuuzia mtu ardhi katika maeneo ya Kibondeni ambayo ni mali ya serikali.

Kamanda Nassir, alisema ardhi hiyo waliiuza kwa shilingi 6 milioni ambapo mlalamikaji alipotaka kuanza shughuli zake katika eneo hilo akabaini kuwa ardhi hiyo haiwezi kutumika.

Alibainisha kuwa, mlalamikaji alidai kuwa aliiuziwa kiwanja hicho Machi 8 mwaka huu saa 4:00 asubuhi lakini alishituka baada ya kuletewa hati ya mauziano ambayo ilionesha ameuziwa na Simai Mwita huku tarehe ya mauziano ikionesha kuwa Machi 17 mwaka 2011 huku Issa Mwinyi akiwa kama shahidi katika hati hiyo.

Hata hivyo, Kamanda Nassir alifahamisha kuwa, wakati mtuhumiwa huyo yupo ndani walipokea taarifa nyengine ya kujitokeza mlalamikaji mwengine alietambulika kwa jina la Salum Saleh Abdul-rahamu (28) ambae aliuziwa kiwanja na Halima kwa shilingi 2.5 milioni ambacho sio cha kwake.

Alisema jeshi lake linaendelea na upelelezi wa matukio hayo na majalada kuyapeleka kwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ili taratibu za kumpeleka mahakamani ziendelee.

chanzo, znzleo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top