RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Tume ya Mipango kufahamu mahitaji ya serikali kwa kila fani na kwa kila mwaka.

Kwa kufanya hivyo, serikali itafahamu idadi halisi ya wanafunzi wanaohitajika na kuweza kujua namna ya kuwaajiri vijana, vyenginevyo wakifundishwa vijana bila ya mpango serikali itajikuta ina idadi kubwa ya wahitimu bila ya ajira.

Aliyasema hayo jana katika mahafali ya kumi na tatu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), katika ukumbi wa chuo hicho Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alitoa indhari hiyo ili kuepuka kupata matatizo ya kuwa na wasomi wengi ambao hatimae watakuwa hawana kazi za kufanya.

“Lazima tuwe na malengo na mipango madhubuti,tusifanye kwa pupa, kasi wala papara,”alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kukiagiza chuo hicho kushirikiana na BAKIZA pamoja na taasisi mbali mbali zinazoshughulikia maendeleo ya Kiswahili katika kuimarisha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni Zanzibar na kukitaka chuo hicho kujiandaa, kujitangaza na kujitahidi ili maendeleo yanayotarajiwa yapatikane.

Agizo hilo limekuja baada ya kuwepo idadi ndogo ya wanafunzi wa kigeni chuoni hapo ambayo haitoi picha nzuri kwani inaonesha idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaojiunga inashuka mwaka hadi mwaka badala ya kupanda hasa ikitiliwa maanani kuwa Zanzibar inategemewa kushika usukani wa kukuza lugha ya Kiswahili.

Hivyo, alieeleza kuwa SUZA kupitia Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni lazima ifanye utafiti na kuandaa mikakati itakayosaidia kukiimarisha Kiswahili na kuongeza idadi ya wanafunzi wa nje wanaojiunga na masomo ya lugha ya Kiswahili.

Aliwatoa wasi wasi wanafunzi wote waliofaulu na wanaoendelea kusoma shahada ya afya ya mazingira,  kwamba serikali inashughulikia suala la mafunzo ya mazoezi na kuiagiza Kamati ya Wataalamu wa Wizara ya  Elimu na Mafunzo ya Amali, SUZA na Wizara ya Afya, zikutuane ili mazoezi hayo yaanze hivi karibuni hapa Zanzibar.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top