MKUTANO wa tisa wa Baraza la tisa la Wawakilishi, unatarajiwa kufanya mambo manane ikiwemo maswali na majibu 74 na miswada mitatu iliyowasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Disemba 2017.
Katibu wa baraza hilo, Raya Issa Mselem, alieleza hayo jana wakati akitoa taarifa ya shughuli za mkutano huo, Chukwani.
Alisema mkutano huo unatarajiwa kuanza kesho, saa 3:00.
Alisema shughuli nyengine zitakazofanywa ni kuwasilisha ripoti tatu ikiwemo ripoti ya serikali kuhusu maombi ya wananchi wa Kisakasaka juu ya namna wanavyoweza kufaidika na machinjio ya wanyama yaliopo eneo lao, ripoti za kamati za kudumu za baraza hilo kwa mwaka 2017/2018 na hoja binafsi juu ya uwekaji wa miundombinu bora kwa watu wenye ulemavu.
Shunguli nyengine, ni uwasilishaji taarifa ya Wawakilishi watano wanaoliwakilisha Baraza katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ripoti ya mwelekeo wa mpango wa taifa.
Kuhusu ripoti ya serikali ya maombi ya wananchi wa Kisakasaka, alisema wananchi hao wametimiza haki yao ya msingi ambayo imezingatia sheria.
Aidha alisema wananchi hao waliomba kupatiwa shilingi 1,000 kwa kila mnyama atakaechinjwa ili zisaidie katika uimarishaji wa maendeleo.
Akizungumzi miswada mitatu, alisema ni pamoja na muswada wa sheria ya kufuta sheria za kusimamia mwenendo wa biashara na kumlinda mtumiaji Zanzibar namba 2 ya mwaka 1995 na kutunga sheria mpya ya ushindani halali wa biashara na kumlinda mtumiaji,kuweka masharti bora zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Alisema muswada mwengine ni wa sheria ya kufuta sheria ya adhabu na kutunga sheria mpya ya adhabu, kwa kuweka masharti bora zaidi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Muswada mwengine ni wa kufuta sheria ya mwenendo wa jinai namba 7 ya mwaka 2004 na kutunga sheria mpya ya mwenendo wa jinai, kuweka utaratibu bora wa upelelezi wa makosa ya jinai na usikilizaji wa kesi za jinai na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment