UONGOZI wa kikundi cha taarab asilia cha Culture umetoa hadi Febuari 15 kwa wasanii Hama Q na Dogo Aslay, wawe wamefika kufanya nao mazungumzo kabla hawajawafikisha mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari Katibu Mkuu wa kikundi cha Culture Taimour Rukuni Taha huko Vuga, alisema kuwa wameamua kutoa hadi tarahe hiyo ili kufanya mzungumzo baada ya wasanii hao kufanya makosa ya kuimba nyimbo zao bila ya ruhusa ya kikundi.
Alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wasanii na vikundi vya muziki kupiga nyimbo zao bila ya ruhusa, jambo ambalo wanalichukia na kuanzia sasa hawapo tayari kuona hali hiyo inaendelea na watu kuzidi kujinufaisha kinyume na utaratibu.
Alisema kuwa wasanii Hama Q na Mosi Suleiman waliimba nyimbo ya (Uke wenza), wakati msanii Dogo Aslay yeye aliimba wimbo wa (Sabalkheri mpenzi) bila ya idhini ya kikundi hicho.
”Wasanii hawa wamejipatia pesa nyingi sana na umaarufu, sisi Culture kwa kweli hatujapendezwa na jambo hilo, hivyo tumetoa mpaka tarehe hizo ili waje tukae nao pamoja na tufanye mazungumzo tukubaliane, la kama hawakuja basi tutachukua hatua kali sana za kisheria”alisema.
Alisema kuwa hivi sasa kumekuwa wimbi kubwa sana la baadhi ya wasanii na vikundi kuzipiga nyimbo zao bila ya ruhusa yao hali ambayo hivi hawawezi tena kuivumilia.
”Sheria ya hati miliki ipo, lakini pia katiba yetu ya Culture inaeleza wazi, kifungu cha 6 kinaelezea umiliki wa nyimbo, ambacho kimeweka bayana kuwa nyimbo zote ni mali ya klabu”alifafanua.
chanzo Zanzibar leo
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment