Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa mchango wa sekta ya viwanda, katika Pato la Taifa umefikia TZS. bilioni 487.9 kwa mwaka 2016, ikilinganishwa na TZS. bilioni 417.0 mwaka 2015.  Hili ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka 2015.  Kadhalika, mchango wa sekta ya viwanda katika jumla ya Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 18.1 mwaka 2015 hadi asilimia 18.6 mwaka 2016.

DK Shein aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar, sherehe ambazo zilifanyika jana katika uwanja wa Aman Zanzibar

Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) imeshaidhinisha ujenzi wa viwanda vinne, katika eneo la Viwanda Vidogo Vidogo Amani pamoja na Maruhubi.  Viwanda hivyo vinajumuisha, Kiwanda cha Mafuta ya Nazi, Kiwanda cha Mafuta ya Kupikia pamoja na Kiwanda cha Vipodozi, Kadhalika, ujenzi wa viwanda vitatu vipya vitakavyojengwa huko Fumba umeshaidhinishwa na ZIPA. Serikali itaendelea na juhudi za kushajihisha wawekezaji wa ndani na nje, kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda.

Serikali kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa au kuingizwa Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya wananchi.  Jumla ya viwango 143 vimetangazwa kupitia Gazeti Rasmi la Serikali na vinatumika.   Hadi mwezi Disemba 2017, jumla ya bidhaa 12 zimepatiwa cheti cha matumizi ya alama ya ZBS.    Ujenzi wa Ofisi na maabara za ZBS unaendelea katika eneo la Maruhubi.



Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top