Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa Katika mwaka huu wa tatu, wa kipindi cha pili 2017/2018, cha Awamu ya Saba, Serikali imetekeleza vizuri Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, MKUZA III na Dira ya Maendeleo 2020 na kupata mafanikio ya kuridhisha.


Dk Shain aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi katika sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kilele chake hufanyika kila ifikapo January 12, ya kila mwaka.

 
Alisema Juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi zimewezesha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.  Jumla ya TZS. bilioni 548.571  zilikusanywa katika mwaka 2017 ikilinganishwa na  TZS. bilioni 487.474 zilizokusanywa katika mwaka 2016. Katika mwaka 2017, mapato yameongezeka kwa TZS bilioni 61.097, ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi cha mwaka 2016, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 12.5.  Natoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), kwa juhudi zao katika ukusanyaji wa mapato. 


Alisema kwa upande mwengine, Pato la Taifa limeongezeka kutoka thamani ya TZS. bilioni 2,308 mwaka 2015 na kufikia thamani ya TZS. bilioni 2,628 kwa mwaka 2016.  Pato hii lilikadiriwa kufikia TZS. bilioni 2,827, mwaka 2017, kwa bei za soko. Katika jitihada tulizoanza kuzichukua mwaka 2011/2012, hivi sasa, utegemezi wa bajeti yetu kwa mwaka 2017/2018, umefikia asilimia 7.3, ikilinganishwa na asilimia 30.2 katika mwaka 2010/2011.  Mafanikio haya tuliyopata ni makubwa na ya kupigiwa mfano.



Kasi ya ukuaji wa uchumi wetu kwa bei halisi, imekua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2017, ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016.  Aidha, Pato la Mtu Binafsi nalo limeongezeka na kufikia TZS.  1,806,000 ikilinganishwa na TZS 1,632,000 kwa mwaka 2015.   Kasi ya mfumko wa bei ilifikia asilimia 5.6 katika mwaka 2017 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2016. Lengo letu ni kuimarisha uchumi, kupunguza umasikini na kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kiwango cha kati ifikapo mwaka 2020.



Alisema katiika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2017 jumla ya miradi 25 iliyopangwa kuingiza mtaji wa US$ milioni 276.84 iliidhinishwa na Serikali. Miradi hii itakapokamilika inategemewa kutoa ajira  zisizopungua 915. Katika mwaka 2017, ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Fumba na Nyamanzi imeendelezwa, kwa lengo la  kuimarisha maisha ya wananchi na kubadilisha taswira ya Zanzibar.  Jumla ya nyumba 170 zimejengwa katika Mradi wa ujenzi wa “Fumba  Satellite City” na nyumba 60 katika Mradi wa “Fumba Town Development”, Nyamanzi.


Kadhalika, mradi wa nyumba za kisasa katika eneo la Mbweni  unaotekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) wa ujenzi wa majengo 18 yenye urefu wa ghorofa 7 unatarajiwa kukamilika, hivi karibuni.  Vile vile,  mradi wa  ujenzi wa hoteli ya kisasa ‘Verde’  ya nyota tano, inayojengwa huko Mtoni Unguja ambao unaotekelezwa na Kampuni ya SS Bakhressa, umekamilika. Hatua inayofuata ni ya uwekaji wa samani. Mradi  huu unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.


Uimarishaji wa miji yetu umeendelezwa kupitia mradi mkubwa wa Huduma za Jamii Mijini (Zanzibar Urban Services Project – ZUSP). Awamu ya kwanza ya Mradi huu, imeshatekelezwa kwa mkopo wa US$ milioni 38 kutoka Benki ya Dunia ambapo ulijumuisha ujenzi wa miundombinu mbali mbali, ikiwemo misingi ya maji, uwanja wa Mnazi Mmoja, majengo, ununuzi wa magari kwa Unguja na Pemba na ujenzi wa ukuta  unaolikinga eneo la Forodhani lisiathiriwe na bahari.  Ujenzi wa  Awamu ya pili ya mradi huu umeshatayarishwa na Benki ya Dunia imekubali kutoa mkopo wa US$ milioni 55.


Huduma za jamii zimeimarishwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).  Jumla ya kaya 32,478 zimepatiwa TZS bilioni 4.45 katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF III.  Vile vile, TASAF III imetekeleza miradi ya kutoa ajira za muda kwa kaya 27,044 Unguja na Pemba.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top