Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Katiba,Sheria,Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haruon Ali Suleiman akibonyeza kitufe kuashiria matumizi rasmi ya  Umeme katika Kijiji cha Mlilile Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

 

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman, amesema mapinduzi ya Zanzibar ndio yaliyowakomboa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kutoka kwenye makucha ya ukoloni.

Akizungumza katika ufunguzi wa mradi wa kupeleka umeme katika kijiji cha Mlilile Matemwe Wilaya ya Kaskazini A ikiwa miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi.

Waziri huyo alisema si vyema kuyapuuza Mapinduzi hayo, akisisitiza wale wanaoyabeza wasipewe nafasi kwani huenda wana ajenda ya siri.

Aidha, aliwataka wananchi wa Unguja na Pemba  kuyaenzi matunda ya Mapinduzi hayo ambayo lengo lake ni kuwainua wananchi wanyonge kwa kuwaletea maendeleo yatakayoinua ustawi wa maisha yao na kuwafanya watembee kifua mbele.

Waziri Haroun alifahamisha kuwa, iko haja kwa wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga nchi, kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haimbagui mtu kwa sura yake au eneo analotoka.

Hata hivyo aliwaomba wananchi wa kijiji cha Mlilile kutumia fursa waliyoipata kwa kutumia huduma ya umeme katika kazi za ujasiriamali pamoja na miradi mingine itakayoweza kuwaingizia kipato.

Akitoa taarifa ya kitaalamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Hassan Ali Mbarouk, alisema serikali imelipa jukumu shirika lake kusambaza huduma ya umeme kwa wananchi hadi katikia maeneo yao popote walipo.

Alisema kazi ya usambazaji umeme vijijini itaendelea kufanywa na serikali hatua kwa hatua ili kuwawezesha wananchi wote kunufaika na huduma hiyo.

Alieleza kuwa, mradi huo katika kijiji cha Mlilile umegharimu shilingi 70,128,721.00 fedha zilizotolewa na Serikali kupitia ZECO.

Alisema utekelezaji wa mradi huo, umefanywa  kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika Mkoa wa Kaskazini mwezi Septemba 2017.

“Katika ziara hiyo, Dk. Shein alitoa agizo la kufikisha umeme kijijini hapa ndani ya kipindi cha miezi sita, lakini ZECO imekamilisha kazi hiyo kwa miezi mitatu tu,” alieleza Mbarouk.

Mradi mwengine kama huo, pia umezinduliwa katika kijiji cha Mbuyumaji Wilaya ya Kaskazini A na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dk. Khalid Salum Mohammed, ambao umegharimu shilingi 79,000,000, ikiwa miongoni mwa shamrashamra hizo za Mapinduzi.

 

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top