RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, jana aliungana na vijana na wanafunzi walioshiriki katika maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar, katika chakula cha mchana alichowaandalia.
Hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya KVZ Mtoni mjini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na baadhi ya viongozi wa vikosi vya SMZ.
Katika shukrani zake kwa vijana na wanafunzi hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu, aliwapongeza kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo sambamba na kufanikisha vyema sherehe hizo zilizofanyika Januari 12, 2018 katika uwanja wa Amaan.
Aliwashukuru walimu, wakufunzi, wasimamizi na washiriki wote katika shughuli za halaiki ambazo zilipamba sherehe hizo.
Alisema ushiriki wao katika sherehe hizo ni dalili njema na mwenendo mzuri wa uzalendo kwa nchi yao huku akieleza imani yake kuwa vijana hao wataendelea kuyaenzi na kuyalinda mapinduzi kutokana na umuhimu wake mkubwa katika maisha ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Alisisitiza haja ya kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini ikiwa ni kielelezo cha kuendelea kuyalinda na kuyaenzi mapinduzi.
Dk. Shein amekuwa na utamaduni wa kuwaandalia chakula vijana na wanafunzi wanaoshiriki sherehe za mapinduzi kila mwaka.
Hafla kama hiyo inatarajiwa kufanyika leo kwa vikosi vya ulinzi na usalama, hafla ambayo itafanyika makao makuu ya KVZ Mtoni.
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment