LICHA ya serikali kuagiza watu wanaoishi kwenye nyumba za kiwanda cha sukari Mahonda kuondoka ili kuwapisha wafanyakazi wa kiwanda hicho, bado agizo hilo halijatekelezwa.
Ofisa habari wa wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Abdalla Abdul-rahman Mfaume, alisema kuwa bado agizo hilo halijatekelezwa.
Alisema zaidi ya miezi mitatu sasa tokea kupeleka barua za kuwataka watu hao kuondoka lakini hadi sasa hakuna hata mtu mmoja alierejesha ufunguo hali ambayo inaonesha dhahiri kuwa wanakaidi agizo la serikali.
Alisema katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa kuna kamati mbalimbali zimeundwa ikiwemo kamati ya kitaifa na wilaya.
Alisema, kamati ya wilaya imefanya jitihada za kuwajuilisha wananchi umuhimu wa kuhama katika nyumba hizo pamoja na kuunda kamati ndogo ya ukarani kwa ajili ya uhakiki wa nyumba hizo.
Alisema uhakiki huo ulibaini kuwa wengi wanaoishi katika nyumba hizo wapo kinyume na utaratibu.
Alisema uhakiki huo ulionesha kuwa nyumba 34 zinakaliwa na familia za wafanyakazi wastaafu waliokuwa wakifanya kazi katika kiwanda hicho siku za nyuma, 12 zinakaliwa na wafanyakazi wa serikali na nyumba tisa wanakaa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema nyumba 50 zinakaliwa na makundi tofauti wakiwemo wananchi wa kawaida, 19 zinakaliwa na wafanyakazi na nyumba 13 zinakaliwa na wataalamu wa kiwanda waliopo sasa.
Alisema uhakiki huo pia ulibaini kuwa nyumba mbili ni mbovu na hazikaliki, moja ilikuwa skuli ya maandalizi, mbili zinatumika kama klabu ya michezo na sanaa na nyumba mbili maghala.
Alisema hawajagundua nyumba iliyouzwa bali kilichogundulika baadhi ya wananchi kuzikodisha kinyume na utaratibu.
chanzo, Zanzibar leo
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment