WAAJIRI wa hoteli za kitalii nchini wametakiwa kuwafanyia uchunguzi ikiwemo kuchukua alama za vidole za wafanyakazi wao kabla ya kuwaajiri na kuweka kamera za usalama (CCTV) ili kupunguza wimbi la uporaji kwa watalii wanaofika katika hoteli zao.
Ombi hilo lilitolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Unguja, Hasina Ramadhan Taufiq, wakati akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Mahonda.
Alisema matukio ya wizi kwa wageni ndani ya vyumba vyao katika hoteli za kitalii yamekuwa yakiongezeka na imegundulika kuwa wahusika wakuu ni wafanyakazi wa hoteli.
Jambo la msingi kwa waajiri hao kufika makao makuu ya polisi kuchukulia alama za vidole za wafanyakazi wao ili iwe rahisi kuwabaini wahusika wa matukio hayo.
Alisema, mkoa wa kaskazini ni moja ya mkoa yenye hoteli nyingi za kitalii na wafanyakazi wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi hali ambayo inaweza kuporomosha soko la utalii nchini.
“Tukumbuke kuwa utalii ni nguzo muhimu katika nchi yetu, hivyo waajiri wakiendelea kuwalea wizi basi watalii wanapoibiwa na kuondoka nchini wanapeleka sifa mbaya na kusababisha kukosa mapato yanayotokana na sekta hii,” alisema.
Alisema Januari 19 mwaka huu baina ya saa 2:30 asubuhi na saa 2:00 usiku katika chumba cha mgeni Wu Chuming raia wa China kuliibiwa dola za Marekani 30,000 sawa na shilingi milioni 67 katika hoteli moja iliyopo kijiji cha Nungwi.
Alisema fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye sanduku lilikokuwa limefungwa kwa kufuli.
Alisema jeshi la polisi linawashikilia baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo ambapo mmoja wao alikutwa na baadhi ya fedha na funguo.
Katika hatua nyengine, alisema Januari 21 mwaka huu saa 11:15 alfajiri mtu mmoja alikutwa amefariki dunia katika kijiji cha Kinyasini Mdodo Pilau akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
chanzo Zanzibar leo
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment