SERIKALI imesitisha utoaji wa pasi za kusafiria (passport) za jumla za makundi mpaka pale utakapopatikana utaratibu rasmi na mzuri kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya nchi husika.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, kufuatia kuwepo kwa mikasa ya kunyanyaswa, kutumikishwa na kuteswa kikatili  kwa baadhi ya Watanzania wanaokwenda nje ya nchi kwa jili ya kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kazi za ndani.

“Nimezipata taarifa hizo za mateso ya watu wetu wanaokwenda nje ya nchi kwa kazi tofauti, nasimamisha utoaji wa paspoti za jumla za makundu ya vijana ambao wamekuwa wakikutana na mikasa hiyo ya kunyayaswa, kutumikishwa, kuteswa kikatili na wengine kuwekwa rehani kwa masuala ya dawa za kulevya. Tunasimamisha mpaka pale tutakapokuwa tumeweka utaratibu ulio rasmi na utaratibu mzuri kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya nchi husika ambako kutakuwa na mahitaji ya namna hiyo,” alisema.

Alieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuwanusuru vijana wa Tanzania kutokana na mateso na ukatili ikiwamo kuwekwa rehani kwa dawa za kulevya pamoja na kunyang’anywa paspoti na kutumikishwa.

Vilevile alieleza kumekuwa na tabia ya watu kuingiza raia wa kigeni nchini na wanapowaingiza wanawafanyisha shughuli nyingine ambazo ni tofauti na zilizopo kwenye vibali vyao, huku akiwataka wote wanaofanya hivyo kuripoti.

“Wako raia wanaoingia kwa makundi nchini kwetu na wale wanaowaleta wanatumia sababu tofauti wanapowaleta na wanapoingia wanawafanyisha shughuli tofauti na walizoombea vibali. Watu wote wanaoomba vibali na baadae wakatumia vibali hivyo tofauti ama wakafanya majukumu mengine tofauti na waliyoombea vibali, wanavunja sheria na watafika kwenye mkono wa sheria,” alisema.

“Watu hawa naelekeza leo (jana) waripoti kwa kamishna wa mipaka na kamishna wa vibali na kama mpaka jioni watakuwa hawajaripoti, wakamatwe na wafike kwenye mkono wa sheria, ili sheria iweze kufuata mkondo wake,” aliongeza.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top