USIKU wa Disemba 31 mji wa Unguja ulikumbwa na tatizo la upungufu wa petroli na kutia dosari sherehe za mkesha wa mwaka mpya, zilizofanyika katika mji mpya wa Fumba Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Gazeti hili lilishuhudia vituo vingi vya kuuzia mafuta vikiwa havina petrol na vichache vilivyokuwa nayo vilikuwa na foleni kubwa na baada ya muda mfupi vilikatisha kuuza bidhaa hiyo.

Hali hiyo ilitoa nafasi kwa baadhi ya vijana kuuza petroli kwa njia ya vidumu kwa bei ya shilingi 4,000 kwa lita badala ya shilingi 2,240 kwa bei halali.

Mmoja ya wauza mafuta katika kituo cha kampuni ya Zanzibar Petroleum, ambae hakutaka jina lake litajwe alisema, tatizo hilo limesababisha na kuchelewa kuwasili kwa meli ya mafuta.

Alisema meli hiyo inatarajiwa kuwasili Zanzibar Jumamosi ya Januari 6 kwa ajili ya kushusha bidhaa hiyo.

Upungufu huo ulisababisha wananchi wengi ambao walipanga kwenda Fumba katika sherehe za kuuaga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka 2018, kukatisha safari yao kutokana na vyombo vyao kutokuwa na mafuta.

Katika viwanja vya Fumba ambavyo sherehe hizo zilifanyika hakukuwa na idadi kubwa ya watu kama ilivyotarajiwa huku vyombo vinavyotumia petroli vikiwa vichache tofauti na ilivyokuwa kwenye sherehe za sikukuu ya Eid al Hajj mwaka jana, ambazo pia zilifanyika katika mji huo.

Tatizo la upungufu wa bidhaa hiyo limeendelea kushuhudiwa hadi jana ambapo vituo vimekuwa vikiuza mafuta ya dizeli ambayo hutumiwa zaidi na gari kubwa  na mafuya ya taa yanayotumiwa kwa matumizi ya nyumbani.

Hata hivyo, taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, imesema hakuna uhaba wa mafuta wowote wa mafuta.

Taarifa hiyo imesema akiba ya mafuta ya petroli iliopo ni lita 624,802 ambazo zinaweza kutosheleza hadi kesho huku mafuta ya dizeli yaliyopo ni lita 1,383,896 sawa na mahitaji ya siku 9.

Aidha taarifa hiyo imesema mahitaji ya mafuta ya petroli kwa siku ni lita 165,000, dizeli lita 152,000 na mafuta ya taa lita 163,000.

Chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top