WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, amesema serikali imejipanga kutoa huduma muhimu kwa wananchi bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.

Alisema hayo katika kijiji cha Sizini wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la kituo cha afya cha Sizini ikiwa ni shamrashamra za miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema lengo la serikali ni kutoa huduma kwa wananchi wake pamoja na kuwapungumzia mzigo mkubwa wa masafa ya kutafuta huduma hizo, kazi ambayo haibagui itikadi ya mtu.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kutokana na uongozi wake ulio thabiti kwa kuwaletea maendeleo wananchi.

“Zanzibar ni ya kwanza kwa upande wa Afrika ya Mashariki pamoja na jangwa la Sahara kuwapatia huduma ya afya wananchi wake tena kwa masafa mafupi sana,”alisema.

Alisema kwa upande wa barabara, serikali imepiga hatua kubwa kuzitengeneza barabara zote za Unguja na Pemba pamoja na kuwapelekea wananchi wote huduma muhimu za kijamii.

“Serikali inajitahidi kuwapelekea wananchi wake maendeleo katika nyanja zote kwani tumeona kipindi hii kifupi tu Dk. Shein amefanya mabadiliko makubwa katika ununuzi wa karafuu na kuongeza bei ili wananchi wanufaike,” alisema.

Naibu Waziri wa Afya, Harous Said Suleiman, alisema wananchi wa Pemba, wana kila sababu ya kujivunia kwani awali walikuwa hawana muda wa kukaa pamoja.

“Tumshukuru Dk. Shein kutokana na juhudi zake anazozifanya kwa kuwaunganisha wananchi wa visiwa hivi pamoja na kuwapelekea maendeleo,”alisema.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Halima Mohamed Salim, alisema kituo hicho baada ya kukamilika kitatoa huduma mbali mbali zikiwemo za uzazi.

Chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top