Baadhi ya maeneo ambayo yaliathirika vibaya kufuatia mvua zilizonyesha katika maeneo mbali mbali 
Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar imekutana na uongozi wa Shirika la Bima Zanzibar kuangalia namna bora ya uanzishaji wa bima ya mafuriko kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaothiriwa na mafuriko katika kipindi cha msimu wa mvua zinazonyesha nchini.

kufuatia kikao maalum cha watendaji wa taasisi hizo kilichofanyika katika ukumbi wa Shirika la Bima Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Shaaban Seif Mohamed ameleza  kuwa Zanzibar kama kisiwa imekuwa ikikumbwa na maafa mbali mbali ikiwemo mafuriko hali inayosababisha uharibifu wa makazi ya watu na mali zao kila ifikapo kipindi cha mvua.

Aidha, Mkurugenzi Shaaban amesema  kuna haja kwa uongozi wa Shirika la Bima kuangalia jinsi gani unaweza kuanzisha bima hiyo ili kuwafidia wananchi wanaopatwa na maafa ya mafuriko ya mvua.

“Kutokana na mafuriko  yanayowakumba wananchi kuna haja kwa Shirika la Bima kuangalia uwezekano wa kuanzisha Bima ya mafuriko ili isaidie kutoa fidia kwa Jamii” Alieleza Mkurugenzi Shaaban.

Mkurugenzi masoko wa Shirika la Bima Said Abdalla amesema amefurahishwa na uongozi wa kamisheni ya maafa kufika katika afisi za shirika la bima kwani ziara hiyo imetoa tija kwa taasisi hizo kuweza kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo mafuriko.

pamoja na mambo mengine Mkurugenzi masoko wa Shirika la Bima ametoa wito kwa waanchi kujenga utamaduni wa kujikatia bima pamoja na mali zao kwa ajili ya kupata fidia kutokana na maafa yanayowakumba, huku akihimiza wananchi kuacha tabia ya kujenga katika maeneo hatarishi kwani katika mfumo huo wa ujenzi holela shirika halitotoa fidia kwa watu waliojenga katika maeneo.

Nae Afisa Mipango kutoka kamisheni ya maafa Mudrik Abdulla Mussa amesema kuna umuhimu mkubwa kwa shirika la bima kuanzisha utaratibu wa bima ya mafuriko kutokana na hali ya sasa kila ifikapo kipindi cha mvua za masika wananchi waliowengi hasa wa kipato cha chini kuathiriwa na mafuriko hali inayopelekea upotevu wa makaazi ya watu na mali zao.

katika majadiliano hayo   taasisi zote mbili kwa kushirikiana pamoja zimekubaliana kufanya tafiti  kwa lengo la kugundua uhitaji wa wananchi samamba na shirika la bima kuweza kutoa huduma ya fidia kwa watu wanaopatwa na maafa.

chanzo, Zanzibar 24

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top