MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan,  amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya masoko ili kuongeza thamani ya  mazao  na kuimarisha huduma za kifedha kwa wananchi vijijini.

Alisema wakulima wengi wa vijijini bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za uzalishaji duni, uwezo mdogo ya kujiwekea akiba pamoja na ukosefu wa masoko ya kuuzia bidhaa zao.

Alisema hayo wakati akifungua soko la kisasa la samaki na mboga mboga shehia ya  Konde wilaya ya Micheweni ikiwa ni shamra shamra za kutimia miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema ujenzi wa soko hilo la kisasa ni mojawapo wa juhudi za serikali za kuwasaidia wakulima hasa wanaoishi maeneo ya vijijini kuweza kukabiliana na changamoto ya masoko na kuwafanya waongeze tija, kipato na kuwa na uhakika wa chakula.

“Ujenzi wa soko hili ni moja wapo wa juhudi za serikali ya kuwasaidia wakulima hasa wa vijijini kuwa na uhakikisha wa kupata soko na haya yametekelezwa ili kutimiza azma ya mapinduzi ya mwaka 1964,”alieeleza.

Aidha alisema serikali zote mbili zitaendelea kutafuta na kutekeleza miradi itakayosukuma mbele maendeleo ya wananchi kwa maslahi mapana ya taifa ili kuwaletea wananchi mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Aliongeza kwamba serikali inatekeleza sera zenye muelekeo wa kupunguza umaskini na kwamba jitihada hizo ni ajenda kuu ya taifa  ambazo zinaweka mazingira bora kwa wananchi ili waweze kujiletea maendeleo.

Mapema Waziri wa Kilimo,Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed alisema serikali inatekeleza miradi ya maendeleo kwa lengo na kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake bila ya upendeleo.

Akitoa maelezo ya ujenzi wa soko hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi,  Joseph Abdalla Meza, alisema  mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 728 mbazo zimetolewa na serikali.

Ujenzi wa soko hilo umetekelezwa na kusimamiwa na Mpango ya Mioundombonu ya Masoko (MIVARF) na kujengwa na kampuni ya Kiure Engineering ya Arusha,chanzo Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top