WANANCHI wametakiwa kuacha dhana potofu ya kuishutumu Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwamba inabadilisha matokeo ya uchunguzi wa dawa za kulevya kama inavyodaiwa, kwani inafaya kazi kwa kuzingatia uadilifu.

 

Mtalaamu Mwandamizi wa ofisi hiyo, Khamis Rashid Kheir, aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo katika maonesho ya biashara yanayoendelea viwanja vya Maisara mjini Unguja.

 

Aidha alisema ofisi yao inafanya kazi kwa umakini zaidi katika kutenda haki na wala haichakachui matokeo ya vielelezo vya dawa za kulevya pale zinapopelekwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi.

 

“Tunapata malalamiko kuwa tunabadilisha matokeo hasa ya dawa za kulevya, sisi tunapofanya uchunguzi tunatoa taarifa sahihi na sio kufanya udanganyifu,”alisema.

 

Akizungumzia kuanzishwa kwa sheria ya udhibiti wa kemikali, alisema kwa kiasi kikubwa imepunguza matumizi mabaya ya kemikali kwa wananchi kwani awali kabla ya kutokuwepo sheria hiyo, Zanzibar kulikuwa na matukio mengi ya matumizi mabaya ya kemikali.

 

Alisema, kulikuwa na matukio mengi ya watu kumwagiwa tindikali lakini hivi sasa kuna udhibiti mkubwa wa uingizaji na utumiaji wa kemikali jambo ambalo limeondosha kabisa matukio hayo.

 

Akizungumzia maonesho hayo ya biashara, alisema kuwa maonesho yametoa fursa kwa wananchi kujionea na kujifunza mambo mbalimbali.

 

“Maonesho haya yamezingatia ubora na kuwatambulisha wananchi juu ya kazi zinazofanywa na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi,”alisema.

 

Hata hivyo, alisema mwitiko wa wananchi kutembelea maonesho hayo ni mzuri na hata wajasiriamali wamepata fursa ya kutangaza na kuuza bidhaa zao.

 

Hivyo, fursa hiyo kuwaomba wananchi kuacha kujibweteka na badala yake watafute shughuli ambazo zitawaongezea kipato na kujikwamua na umasikini.

 

“Kuna watu wengi ambao wamejitokeza kuonesha ujuzi wao kupitia kazi za mikono na kupata faida kwa bidhaa wanazozitengeneza na kupata fedha kwa ajili ya kujikimu na maisha,” alisema.

Chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top