Ndugu wa Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji, Vicenti Mughwai alisema jana kuwa afya ya kaka yake Lisu  inazidi kuimarika na sasa anaweza kufanya mambo mengi mwenyewe ikiwamo kwenda kuoga na kutembea kwa kutumia magongo.


Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), alipelekwa Ubelgiji Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

 

“Tunamshukuru Mungu sana, Lissu anaendelea vizuri… tangu ameanza kupatiwa matibabu na mazoezi ya viungo tunaona mabadiliko makubwa mno, “Maendeleo ni makubwa sana, kuna vitu alikuwa hawezi kuvifanya lakini sasa anaweza kuvifanya mwenyewe kama kuoga. Siku za nyuma alikuwa akipelekwa maliwatoni lakini sasa hivi anatembea na magongo mwenyewe kwa kukanyagia mguu chini, Anakula mwenyewe.Tunaamini atatengamaa mapema zaidi, (na) haya kwetu ni maendeleo makubwa.” alisema Vinceti Mghwai.

 

Alisema Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa Hospitali ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu waliokuwa wakienda kumjulia hali.

 

“Kwa sasa ana muda wa kutosha kufanyiwa matibabu ya mazoezi, madaktari wanamfanyia mazoezi muda wote kwa sababu hakuna watu wanaokwenda kumuona na ndiyo sababu anaendelea kupona haraka,” alisema Mghwai.

 

Kuhusu risasi iliyobakia kwenye nyonga, Mghwai alisema madaktari wa Ubelgiji hawataitoa na wataiacha kwa sababu walishaeleza kuwa haiwezi kuwa na madhara kwake kiafya.

 

Mghwai alisema, zaidi ya Sh. milioni 100 zinatumika kila mwezi kwa ajili ya kumtibu na kwamba hadi sasa Bunge halijatoa fedha na familia inafuatilia lakini wamekuwa wakizungushwa huku na kule.

 

Alisema fedha zinazotumika kwa ajili ya matibabu yake ni zile zilizochangwa na wadau mbalimbali ingawa hazitoshi na kwasasa wadau wamesitisha kutoa michango baada ya tetesi kuwa serikali inagharamia matibabu yake.

 

“Gharama ni kubwa sana kwa mwezi analipia zaidi ya milioni 100 katika hospitali hiyo na kama atakaa miezi miwili tutatumia zaidi ya milioni 200 na hizi ni fedha za matibabu pekee,” alisema Mghwai.

 

Alisema familia inaendelea na juhudi za kuchangisha fedha zaidi ili kukamilisha matibabu yake.

 

“Tunaamini hakuna kitakachoharibika kwa sababu tumeshaweza kumponya tunaamini atakuwa mzima.” 

 

Alisema gharama kamili za matibabu na fedha zilizopatikana kwa ajili ya matibabu ya Lissu zinaweza kuzungumzwa katika vikao vya makubaliano na si yeye peke yake kuzungumzia.

chanzo, Zanzibar 24

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top