WAZIRI wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed, amesema hawezi kuyabeza mapinduzi ya Zanzibar  licha ya kwamba  anatoka  chama cha upinzani cha Alliance Democratic Change (ADC).

Alisema anaelewa umuhimu wa mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo ni mkombozi kwa wazanzibari na ni dira ya  maendeleo kwa wananchi.

Alisema hayo wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua jengo  la  kituo cha huduma rafiki na ushauri nasaha kwa  vijana Bwagamoyo Mtambwe wilaya ya Wete ikiwa ni shamrashamra za miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kuzinduliwa kwa kituo hicho  ni miongoni mwa matunda ya mapinduzi, hivyo ataendelea kuyaenzi, kuyathamini na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kulitunza jengo hilo.

“Upinzani isiwe sababu ya kuyabeza  mapinduzi kwani yamewakomboa wazanzibari kutoka kwenye minyororo ya ukoloni, hivyo nina kila sababu ya kuyaenzi  na kuyasherekea,”alieleza.

Aidha aliwataka wahudumu wa vituo vya afya kutumia lugha ya upole wakati wanapotoa huduma kwa wagonjwa ili kuondoa malalamiko yanayotolewa na wananchi.

Alisema  moja ya sifa za muhudumu na mtuhumishi wa umma ni kutumia lugha ya upole na busara kwa mwananchi.

Alisema serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya mapinduzi ya Januari 1964, hivyo haitakuwa jambo la busara kwa watumishi wa umma kutoa maneno mabaya na ya kashfa kwa wagonjwa.

“Tumieni lugha ya upole na hekima wakati wa kutoa huduma, hii itawafanya wananchi kuzidisha imani kwa serikali yao pamoja na huduma zinazotolewa kwenye kituo hiki,”alisema.

Mapema akisoma risala, Ofisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba, Bakar Ali Bakar, alisema moja ya majukumu ya kituo hicho ni kutoa elimu ya uzazi wa mpango pamoja na kutoa ushauri na nasaha kwa vijana.

Chanzo, Zanzibar leo

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top