RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameagana na Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT) anayemaliza muda wake Profesa Benno Ndulu ambaye ameeleza furaha yake kwa kuona uchumi wa Zanzibar ukiwa umeimarika kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wa Dk. Shein.

Katika mazungumzo hayo ya kuagana yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Profesa Ndulu alimueleza Dk. Shein kuwa kazi ya kuimarisha uchumi iliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein ni kubwa sana na kuna haja ya kupongezwa.

Kwa upande wa sekta ya utalii alisema imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar  na kupelekea kuimarika kwa huduma mbali mbali za kijamii badala ya kutegemea zao moja la karafuu peke yake.

“Nuru ya Zanzibar inaendelea kungara na maendeleo yanazidi kuimarika siku hadi siku…hongera sana kwa hatua ya kiuchumi iliyofikiwa hapa Zanzibar, pongezi hizi nazitoa kwa dhati ya moyo wangu kabisa”, alisisitiza Profesa Ndulu.

Pamoja na hayo, Profesa Ndulu alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein mashirikiano mazuri yaliopo kati ya uongozi wa Wizara ya Fedha Zanzibar na Benki hiyo hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa ndani ya uongozi wa miaka kumi akiwa Gavana wa BoT na matarajio aliyonayo ya kuendeleza zaidi mafanikio hayo.

Sambamba na hayo, Profesa Ndulu alimueleza Dk. Shein majukumu yake mengine atakayoyafanya katika masuala mazima ya kiuchumi na kifedha kitaifa na kimataifa mara baada ya kumaliza muda wake wa kazi ya Gavana wa (BoT).

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alimpongeza Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT) anaemaliza muda wake Profesa Benno Ndulu kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kuiimarisha na kuiendeleza sambamba na kusimamia fedha za Tanzania katika Benki hiyo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa (BoT), ni Benki ya Muungano ambayo imekuwa ikifanya vyema shughuli zake kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzani.

Aidha, Dk. Shein Shein alieleza kuwa ipo haja ya kujivunia mafanikio hayo makubwa ya kiuchumi yaliofikiwa hapa Zanzibar huku akieleza matumaini yake ya kuendelea Benki hiyo kufanya vizuri chini ya uongozi mpya wa Profesa Florens Luoga.

Rais Dk. Shein alimueleza Gavana huyo anaemaliza muda wake kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wake itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa na Benki hiyo kupitia Tawi lake lililopo Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

Facebook Blogger Plugin by Piere

Post a Comment

 
Top