RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema, serikali inathamini mchango wa elimu unaotolewa na chuo kikuu cha Sumait, kwa kutoa taaluma ya fani ya sayansi na sanaa kwa walimu wa skuli za serikali na binafsi.
Akizungumza kwa niaba yake katika mahafali ya 17 ya chuo hicho yaliyofanyika Chukwani, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri, alisema chuo hicho ni moja ya vichocheo vya kusaidia kutatua tatizo la walimu serikalini.
Alisema amefurahishwa kusikia kwamba kuna wahitimu 461 ambao wanatunukiwa shahada ya kwanza na wengine 287 kwa ngazi ya stashahada na ceti pamoja na kutoa idadi ya walimu wengi wanaosaidia Zanzibar na sehemu nyengine Afrika.
“Ninaimani wahitimu hao 748 wataingia au kuendelea katika soko la ajira kwani tunahitaji ujuzi wao na michango katika juhudi za kuharakisha maendeleo nchini,” alisema.
Alipongeza uongozi wa chuo hicho kwa juhudi za kulinda hadhi ya chuo kwa kuhakikisha kinatoa elimu bora na kuendesha shughuli zake kwa kufuata miongozo ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Alisema kwa mujibu wa viwango vya vyuo vikuu kwa mwaka 2017,chuo hicho kilishika nafasi ya 31 kwa vyuo vikuu vya Tanzania na kuwa ni miongoni mwa vyuo vikuu bora 200 Afrika.
Alisisitiza kwamba nafasi hiyo iongeze hamasa na ari zaidi katika kutoa elimu bora hasa ikizingatiwa kina uwezo wa kulinda hadhi ya chuo ili kiwe na viwango bora zaidi.
Alisema katika kukabiliana na ushindani wa elimu ya vyuo vikuu ipo haja ya kutafuta programu zitakazowezesha kupanua soko ili kupata wanafunzi wengi zaidi.
Alisema serikali inaendelea kutoa na kuimarisha elimu bure kwa wanafunzi wa msingi na sekondari huku ikihakikisha kila mtoto anapata fursa sawa katika kutimiza ndoto zao.
chanzo, Zanzibar leo
Facebook Blogger Plugin by Piere
Post a Comment